Habari za Punde

MADEREVA, MAKONDAKTA WAPEWE MIKATABA

Na Nafisa Madai

WAZIRI wa Miundombinu na Mawasiliano, Hamad Masoud Hamad amesema wakati umefika kwa madereva na makondakta kuwa na mikataba itakayolinda na kuhakikikisha wanapata haki zao.

Waziri huyo alibainisha hayo alipokuwa akifungua kongamano la kuadhimishwa wiki ya kimataifa ya wafanyakazi wa sekta ya usafiri wa ya barabara huko katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Mnazimmoja mjini hapa.


Alisema huu si wakati kwa makondakta na madereva wa daladala na taxi kufanya kazi kwa kubahatisha kwani wanapaswa kisheria kufanyiwa mikataba ya kazi kwa vile wanategemea na familia zao.

Aidha alisema kutokana na umuhimu wa mikataba ya kazi wizara yake italishughulikia suala la madereva na matingo wa daladala na kuweza kuona kuwa wanamikataba ya ajira ili kuwa na uhakika wa kazi wanayoifanya.

Waziri huyo alisema mikataba hiyo itawawezesha madereva hao na matingo kupata mapumziko na kufanya kazi kwa mujibu wa kufuata sheria za kazi na kusaidia kupunguza uchovu na kuondosha ajali barabarani za mara kwa mara.

Alisema wizara yake pia itachukua juhudi ya kuimarisha ofisi ya ukakuzi wa magari kwa kuipatia vifaa vya kisasa vya ukaguzi wa magari ili iweze kulingana na teknolojia mpya inayokwenda sambamba duniani kote.

Sambamba na hayo waziri huyo alisema utaratibu maalum unaandaliwa na wizara wa kutoa mafunzo ya kutosha kwa matingo na madereva ili waweze kufanya kazi bora na kuwajali wateja wao na kulinda mali za matajiri zao.

Waziri huyo alisema wizara itaimarisha alama za barabarani, taa,sehemu za kuegesha magari na kusimamia vituo vya uhakika ili kupunguza misongamano isiyo ya lazima.

Kwa upande wake katibu mkuu wa chama cha wafanyakazi wa sekta ya usafirishaji, Muhamedi Ali Salum alisema chama chao kinakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo ukosefu wa mikataba jambo ambalo limekua likiwarejesha nyuma kimaendeleo.

Katibu huyo alisema kutokuwa na mikataba ya kazi wa madereva hao na matingo ndiko kunakosababisha kufanya kazi kinyume na sheria za barabara na kusababisha ajali za mara kwa mara.

Kongamano hilo limewashirikisha wadau mbalimbali kupitia jumuia zao wakiwemo madereva, matingo wa daladala na madereva wa magari ya mizigo na matingo wao madereva wa gari za shamba na matingo wao pamoja na madereva wa taxi ambapo ujumbe wa mwaka huu kimataifa ni usalama sasa (SAFETY NOW) .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.