Habari za Punde

KUTOKA BARAZANI: HATUWEZI KUVUNJA MKATABA NA WAKANDARASI - WAZIRI

SERIKALI haina mpango wa kuvunja mkataba na kampuni iliyopewa kazi ya kujenga barabara kadhaa za Unguja na Pemba kutokana na kuchelewa kumaliza ujenzi wake.

Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Hamadi Masoud, alitoa taarifa hiyo barazani jana wakati akijibu suali la nyongeza la Mwakilishi wa Kwamtipura, Hamza Hassan Juma, aliyetaka kujua kwanini serikali haifikirii kuvunja mkataba na kampuni hiyo, kutokana na kuchelewa kwa kandarasi za barabara hizo.


Waziri huyo alisema serikali haitaweza kuvunja mkataba kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo baadhi ya wadau wa usimamizi wa barabara hizo kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa wakati.

Alisema katika ujenzi huo kumekuwa na makundi matatu ikiwemo ya serikali ambayo hutakiwa kulipa fidia kwa wananchi ambapo barabara hupitishwa na pia upande mwengine wa barabara za mkopo ambapo hutegemea namna ya uingizwaji wa fedha kwa wakandarasi.

Kutokana na kuwapo kwa makundi hayo, Waziri huyo alisema kumekuwa na matatizo yanayojitokeza ya baadhi ya wadau hao kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa wakati.

Hata hivyo, alisema bado serikali itahakikisha inatekeleza utengenezaji wa barabara hizo unafanyika kwa haraka ili ziweze kumalizika.

Mapema, Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Issa Haji Gavu, akijibu suali la msingi la Mwakilishi wa Mtambwe, Salim Abdalla Hamad, aliyetaka kujua kampuni ipi imepewa kazi ya kujenga barabara ya Wete ambapo Naibu huyo alisema ni Kampuni ya Mwananchi Engineering & Consruction Co. (MECCO) ya Dar es Salaam ambapo itasimamiwa na na kampuni ya J.Burrow kutoka Afrika ya Kusini na utatekelezwa kwa awamu mbili.

Alisema ujenzi wa barabara hiyo unatarajiwa kuanza baada ya kukamilika kwa barabara za awamu ya kwanza kutokana na fedha ziliopo zisingetosha kwa ujenzi wa barabara tatu na imeamuliwa kwa sasa kujengwa barabara mbili na ya tatu ianzishiwe utaratibu wa kuombewa fedha.

Aidha Naibu huyo alisema kuhusu suala la ulipaji wa fidia kwa wananchi walioathirika na ujenzi huo tayari serikali imo katika hatua za mwisho kukamilisha taratibu za kulipa fidia hizo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.