Habari za Punde

MAWAZIRI SEKTA YA UCHUKUZI WA SMT NA SMZ WAKUTANA

Nafisa Madai - Zanzibar

Kikao cha Mawaziri wa Sekta ya Uchukuzi wa SMT na SMZ kuzungumzia pamoja na mambo mengine kilikubaliana kuimarisha usimamizi na usalama wa usafiri wa bahari hapa nchini pamoja na kuwa na viwango vya usalama vinavyofanana kwa pande zote mbili.

Kikao hicho cha siku moja kimefanyika kufuatia agizo la Baraza la Usalama la Taifa wakati wa kikao chake cha tarehe 11 Septemba 2011 ambacho kiliagiza Mawaziri wanaosimamia usafiri wa majini wa SMT na SMZ wakutane na kuangalia maeneo yenye mapungufu katika usafiri wa majini ili kuondoa mapungufu hayo.


Mawaziri hao wamesema kuwepo kwa viwango sawa vinavyotumika katika vyombo vya majini ni pamoja na sheria na kanuni zinazotumika kusimamia usalama wa vyombo vya majini nchini na kuwepo vigezo vinavyofanana vya kampuni na taasisi za ukaguzi na taaluma nyingine za meli kunaweza kuleta afueni katika sekta hizo.

Mawaziri hao walisisitiza umuhimu wa kutekelezwa kwa mikataba ya kimataifa ambayo imeridhiwa na nchi kwa kuhakikisha kuwa mikataba hiyo inawekwa katika sheria za nchi hizi mbili kutokana na kuwepo kwa mikataba ambayo imeridhiwa lakini bado haijatungiwa sheria.

Aidha mawaziri hao kwa kauli moja walikubalina kuwepo kwa wafanyakazi wa vyombo vya usafiri wa majini ambao wanasifa na viwango vinavyoendana na kazi za usafiri majini na mikataba na itifaki mbalimbali zilizoridhia za International Maritime Organization (IMO).

Sambamba na hilo Mawaziri hao waliagiza SUMATRA na ZMA kuhakikisha kuwa wafanyakazi wanaofanya kazi kwenye vyombo vya majini wanakuwa na sifa zinazostahili ili kuweza kufanya kazi zao kwa umakini endapo itatokea dharura yoyote kwenye vyombo vyao.

Hata hivyo, waliagiza kuwa taasisi zinazohusika na mafunzo ya wafanyakazi wa vyombo vya majini ziwe na utaratibu wa kupitia mitaala ya mafunzo ya wafanyakazi wa vyombo vya majini mara kwa mara kwa lengo la kuangalia endapo mafunzo yanakidhi hali halisi ya vyombo vya usafiri vilivyomo nchini kwa wakati husika.

Mawaziri hao walisema ipo haja ya kuimarisha huduma za utafutaji na uokoaji (SAR services) kisheria katika ajali zinazotokea majini na angani na kuharakishwe mchakato wa kutungwa kwa sheria ya utafutaji na uokoaji ambayo itahusisha utafutaji na uokoaji wa ajali na kwa upande wa usafiri wa anga.

Kwa upande wa wamiliki wa vyombo vya usafiri majini Mawaziri hao waliagiza kuwa wamiliki hao wahakikishe kuwa wanatekeleza kanuni zote za majini zinazohusu usalama wa vyombo vya majini ili kuepusha ajali zinazoepukika.

Kikao hicho pia kilitilia mkazo utekelezaji wa kanuni za kuhesabu abiria na kutoa taarifa za usalama kwa abiria wanapokuwa safarini ambapo imeonekana kuwa kanuni hizo zipo Tanzania Bara tu ambapo Mawaziri hao waliamuru kanuni kama hizo zitungwe kwa upande wa Zanzibar na kutumika ipasavyo.

Kauli za Mawaziri hao pia iliagiza kuwa SUMATRA, ZMA, ZPC na TPA kuongeza utoaji wa elimu kwa umma juu ya usalama wa usafiri wa majini, anga na nchi kavu kwa kutumia vyombo mbali mbali vya habari, matamasha, vipeperushi mabango warsha na makongamano ili kuongeza mwamko wa usalama kwa umma.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.