KATIBU Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dk.Omar Dadi Shajak amesema upo umuhimu wa kuwepo kwa sera na mikakati itakayohakikisha yanakuwepo makabiliano ya mabadiliko ya tabianchi.
Akizindua kamati ya kitaalamu ya kusimamia mabadiliko ya tabianchi Zanzibar huko ofisini kwake Migombani, Shajak alisema suala la mabadiliko ya tabianchi linamuhusu kila mtu na linagusa nyanja mbali mbali za kijamii zikiwemo uchumi ya afya.
“Mabadiliko ya tabianchi ni dhana pana, sio suala la kiamzingira pekee kama wengi wetu tunavyofikiria, suala hili linagusa maisha ya wananchi wote katika shughuli zao za kilimo, uvuvi, afya, nakadhalika”, alisema Katibu huyo.
Aidha alifahamisha kuwa mabadiliko ya tabia nchi yanatokana na sababu mbali mbali baadhi yao zikiwa haziwezi kuonekana huku zikihitaji utaalamu kuweza kuzigundua.
Alifahamisha kuwa Zanzibar kama zilivyo nchi nyengine duniani inakabiliwa na tatizo hilo la mabadiliko ya tabia nchi, na ndio maana kukawepo na mmomonyoko wa fukwe, kuibuka kwa mashimo katika eneo la Jang’ombe na mafuriko katika maeneo mbali mbali hasa inapofika kipindi
cha mvua kubwa.
Katibu huyo alisema kamati hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi katika kufanikisha majukumu yake na kuwataka wajumbe kuikubali dhamana waliyopewa, ikizingatiwa kuwa hiyo ni dhana mpya katika nchi yetu.
Aliwataka wajumbe wa kamati hiyo kuunganisha nguvu na kuhakikisha kuwa suala hilo linafanikiwa kwa maslahi ya wananchi ya taifa.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati hiyo Fauzia Mwita alisema ushauri wa kitaalamu unahitajika katika kuliendeleza suala hilo, na kwamba kamati hiyo italazimika kutoa taaluma kwa wajumbe wake ili iweze kufanya kazi zao vizuri.
Hatua hiyo imekuja kutokana na wajumbe wengi kulalamika kuwa hawana taaluma ya kutosha kutokana na kuwa dhana ya mabadiliko ya tabianchi ni mpya kwa Zanzibar.
Nae mjumbe wa Sekretarieti ya mabadiliko ya tabianchi Zanzibar, Sihaba Haji Vuai alisema mradi wa maji wa African Adaptation Program (AAP) unaotekelezwa katika kijiji cha Nungwi ni miongoni mwa hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi hapa Zanzibar.
Alisema mradi huo utakapokamilika utaweza kuondoa tatizo la muda mrefu la ukosefu wa maji safi na salama kwa wananchi wa Nungwi kwa vile maji yao yamekuwa yakichanganyika na maji ya chumvi.
Zaidi ya shilingi milioni 500 zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya mradi huo ambapo hadi sasa tayari shilingi milioni 400 tayari zimeshapatikana.
Kamati hiyo ya kitaalamu inaundwa na wakurugenzi kutoka taasisi mbali mbali zikiwemo Kilimo, Mazingira, Misitu, Maji na Mamlaka ya hali ya hewa.

No comments:
Post a Comment