Habari za Punde

TAARIFA KUHUSU TUKIO LA KUZAMA KWA MELI YA M.V. SPICE ISLANDERS ILIYOTOKEA TAREHE 10 SEPTEMBA, 2011 KATIKA ENEO LA MKONDO WA BAHARI YA NUNGWI

1.0. UTANGULIZI:

Mheshimiwa Spika,
Kwa heshima naomba kuchukua nafasi hii kumshuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kukutana hapa leo tukiwa wazima na wenye afya njema. Pili, naomba nichukue nafasi hii adhimu kukushukuru wewe Mheshimiwa Spika, kutupatia fursa hii adhimu ili kuwasilisha mbele ya Baraza lako Tukufu taarifa ya maafa ya kuzama kwa meli ya M.V. Spice Islanders I iliyotokea katika mkondo wa bahari ya Nungwi tarehe 10 Septemba, 2011.

Mheshimiwa Spika,
Meli ya M.V. Spice Islanders I ilitengenezwa mwaka 1974 na kufanyiwa marekebisho makubwa (re-built) nchini Ugiriki mwaka 2001. Meli hii ilinunuliwa na ‘Visiwani Shipping Company’ mwaka 2007 na kupatiwa usajili tarehe 10 Oktoba, 2007 baada ya kufanyiwa ukaguzi kwa mujibu wa Sheria ya Usafiri Baharini ya mwaka 2006 na iliruhusiwa kubeba abiria 600 na mizigo tani 500. Meli hiyo ina urefu wa mita 58.15 na upana wa mita 11.4.


Mheshimiwa Spika,
Mnamo tarehe 10 Septemba, 2011 majira ya kati saa nane na tisa za usiku ilipatikana taarifa ya ajali ya kuzama kwa meli hiyo katika maeneo ya mkondo wa bahari ya Nungwi. Meli hiyo ilikuwa katika safari yake ya kawaida ya kutoka Unguja kwenda Pemba ikiwa imebeba abiria na mizigo. Awali, meli hiyo iliondoka bandari ya Dar es Salaam mnamo saa 5 za asubuhi siku ya tarehe 9 Septemba, 2011 ikiwa imebeba mizigo na abiria kuelekea Wete Pemba kupitia Unguja. Kwa mujibu wa taarifa za Mamlaka ya Bandari Tanzania, meli hiyo ilikuwa na jumla ya abiria 229 (kati yao watoto 63) na mizigo tani 58. Abiria 136 waliotokea Dar es Salaam walikuwa wanaendelea na safari yao hadi Wete Pemba.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mamlaka ya Usafiri Baharini (Zanzibar Maritime Authority), meli hiyo iliondoka Unguja kuelekea Wete Pemba majira ya saa 3.20 za usiku wa tarehe 9 Septemba, 2011 ikiwa imepakia abiria 610 na mizigo tani 95.

Mheshimiwa Spika,
Taarifa hii inaelezea kwa kina juu ya hali halisi ya tukio pamoja na hatua zote zilizochukuliwa kuanzia tarehe 10 Septemba, 2011 hadi hivi sasa.

Mheshimiwa Spika,
Mara baada ya tukio hili, Kamati ya Kukabiliana na Maafa ya Taifa ilikutana usiku huohuo kwa ajili ya kuweka mikakati ya hatua za kuchukua pamoja na kuandaa taarifa rasmi ya Serikali kwa wananchi kupitia vyombo vya habari. Aidha, Baraza la Mapinduzi lilikaa na kutoa maagizo juu ya hatua za kuchukua ikiwemo kutayarisha eneo la Maisara kwa ajili ya Mapokezi na utambuzi wa maiti; kutayarisha eneo la kuzika miili ya marehemu huko Kama; kuweka takwimu sahihi za majeruhi na waliofariki katika ajali hiyo; pamoja na kutolewa kwa taarifa rasmi ya hali ya maafa.

Vile vile, Baraza hilo liliagiza kutangazwa kwa siku tatu za maombolezo; kuwa na siku maalum ya dua ya kitaifa kwa ajili ya waliofariki; kuundwa kwa Kamati ya Viongozi ya kuzifariji familia zilizopoteza ndugu na jamaa zao na kuweka utaratibu mzuri wa kuratibu misaada na michango inayotolewa.

2.0. HATUA ZILIZOCHUKULIWA:

Mheshimiwa Spika,
Kufuatia maagizo hayo ya Serikali, hatua zifuatazo zilichukuliwa:-

1. Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi siku ya tarehe 10 Septemba, 2011 alilitangazia rasmi Taifa kuhusu tukio la kuzama kwa meli na kuwa Taifa liko katika hali ya maafa, pamoja na kutangaza siku tatu za maombolezo.

2. Vituo vya mapokezi ya wahanga wa ajali hiyo vilifunguliwa katika maeneo ya Bandari ya Malindi, Nungwi na Maisara kwa Unguja. Kwa upande wa Pemba vituo vilifunguliwa katika maeneo ya Bandari ya Mkoani, Uwanja wa Gombani Chake Chake na Ukumbi wa Jamhuri Wete.

3. Vikosi vya Ulinzi na Usalama vilipelekwa katika maeneo mbalimbali ili kuimarisha huduma za ulinzi na uokozi wa haraka.

4. Kazi ya uchimbaji wa makaburi katika eneo la Kama ilifanyika kwa mashirikiano makubwa ya Viongozi wa Mkoa wa Mjini/ Magharibi, Vikosi vya Ulinzi na Usalama pamoja na wananchi. Jumla ya makaburi 134 yalichimbwa.

5. Sala na dua maalum ya kuwaombea marehemu wote ilifanyika baada ya sala ya Alaasiri tarehe 12 Septemba, 2011 katika viwanja vya Maisara. Katika sala hiyo wagonjwa waliombewa kupata nafuu ya haraka na wafiwa kuwa na moyo wa subra.

6. Kuorodhesha majina ya wale wote ambao wanasadikiwa walikuwemo ndani ya chombo kilichopata ajali na hadi sasa hawajulikani walipo. Taarifa hizi zinakusanywa kupitia ngazi ya Shehia na Wilaya kwa Unguja na Pemba.

7. Kutoa huduma ya kuwasafirisha majeruhi baada ya kupata matibabu kurudi makwao, na

8. Kutoa huduma za chakula na usafiri kwa walioshiriki katika shughuli nzima za uokoaji.


3.0. MATOKEO YA UOKOAJI:
3.1. Shughuli za uokozi:

Mheshimiwa Spika,
Kutokana na shughuli ya uokoaji iliyofanywa na Vikosi vya Ulinzi na Usalama kwa mashirikiano makubwa ya wananchi hasa wa maeneo ya Nungwi yamepelekea kuwa na idadi ya watu waliookolewa wakiwa hai kufikia 619 na miili ya waliofariki dunia iliyopatikana kufikia 203. Kati ya maiti hizo 197 zilipokelewa kituo cha Maisara na 5 zilipatikana na kuzikwa Mombasa Kenya na moja ilipatikana na kuzikwa Moa, Mkoani Tanga. Mpaka hivi leo hakuna taarifa yoyote ya kupokelewa kwa miili zaidi.

Kwa waliookolewa wakiwa hai waliweza kufikishwa katika Hospitali ya Kivunge, Hospitali ya Jeshi Bububu na Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa uchunguzi na matibabu. Majeruhi wawili kutokana na hali zao walisafirishwa na kupelekwa Hospitali ya Muhimbili. Hadi sasa majeruhi wote wameshatibiwa na kuruhusiwa.

Mheshimiwa Spika,
Katika kituo cha Maisara maiti zilipangwa ili kuwawezesha ndugu na jamaa kutambua maiti wao na kwa kurahisisha kazi hiyo, Shirika la Utangazaji kupitia kituo chake cha Televisheni na Zanzibar Cable Televisheni walichukua picha za sura za marehemu na kuzionyesha zikiwa tayari zimewekewa namba ili kurahisisha utambuzi na uchukuaji wa maiti hao. Kupitia utaratibu huu, jumla ya maiti 158 walitambuliwa na kukabidhiwa jamaa na ndugu zao kwa ajili ya mazishi. Idadi ya maiti ambao hawakutambuliwa ni 39 na mazishi yao yalisimamiwa na Serikali katika eneo la Kama. Kila maiti alizikwa katika kaburi lake chini ya usimamizi wa Masheikh kutoka Ofisi ya Mufti na Wakfu na Mali ya Amana. Jumla ya maiti 6 ambao hapo awali walitambuliwa na jamaa zao pia walizikwa katika eneo la Kama na hivyo kufanya jumla ya maiti waliozikwa katika eneo hilo kuwa 45.

Aidha, katika kituo cha Maisara huduma za uoshaji na sala ya maiti zilitolewa na pia wale wote waliochukua maiti wao walipatiwa sanda na ubao kwa ajili ya kuzikia.

3.2. Juhudi za kuitafuta meli na watu waliokuwa
hawajaonekana:

Mheshimiwa Spika,
Katika jitihada za Serikali za kuhakikisha miili zaidi ya marehemu waliotokana na ajali ya meli inapatikana, Serikali ilipata msaada wa wazamiaji kutoka Afrika ya Kusini. Hivyo, siku ya Jumatatu ya tarehe 12 Septemba, 2011 kikosi cha Jeshi la Wanamaji la Afrika ya Kusini kiliwasili Zanzibar kwa ajili ya kusaidia shughuli za uokoaji katika eneo la tukio. Kikosi hicho kilikuwa na jumla ya askari 22, wakiwemo wazamiaji (Divers) 12, wahudumu wa afya (Medical Staff) 4 na wahudumu wa ndege (Crews) 6. Aidha, kikosi hicho kilikuja na vifaa mbali mbali vya uokozi.

Asubuhi ya tarehe 13 Septemba, 2011, wazamiaji hao kwa kushirikiana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania na Kikosi cha KMKM walifika katika eneo la tukio kwa ajili ya kuanza kazi rasmi. Hata hivyo, wazamiaji hao walishindwa kufanya kazi zao kutokana na kina kirefu cha maji katika eneo hilo ambacho kinakadiriwa kuwa kati ya urefu wa mita 270 hadi 300. Vilevile kwa siku hiyo eneo hilo lilikuwa na mawimbi makali na mwendo wa kasi wa maji (water drifting - 4miles/hr). Aidha, vifaa walivyokuja navyo wazamiaji hao ni vile vinavyoweza kutumika si zaidi ya kina cha maji cha mita 80 tu.

Mheshimiwa Spika,
Vikosi hivyo viliendelea na jitihada za kuitafuta meli na watu waliokuwa hawajaonekana kwa kujigawa katika makundi matatu. Makundi mawili yalihusika na kazi ya utafutaji wa watu katika maeneo ya ukanda wa eneo la tukio kuelekea upande wa Kaskazini, ambao ni Pangani na Ghuba ya Moa Mkoa wa Tanga. Kundi jengine lilijihusisha na kazi ya uzamiaji (diving) kwa ajili ya kusafisha eneo la tukio kwa kina cha mita 50 chini ya bahari ili kuepusha ajali zinazoweza kutokea kutokana na meli hiyo na mizigo iliyokuwemo. Kazi hii ilifanyika ili kusafisha njia kwa meli zinazopita katika eneo hilo na kuepusha ajali nyengine kuweza kutokea.

Wakati kazi za uzamiaji zikiendelea, wazamiaji hao walieleza kwamba meli hiyo ilikuwa chini umbali wa kati ya mita 270 mpaka 300. Hivyo, kutokana na vifaa walivyokuwanavyo hakukuwa na uwezekano wa kuifikia, na hata kama ikifikiwa uwezekano wa kukuta watu wakiwa hai haukuwepo tena na miili yao itakuwa katika hali mbaya sana.

Kutokana na hali hiyo, wataalamu hao waliishauri Serikali kupitia Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa kusitisha rasmi zoezi hilo tarehe 16 Septemba, 2011.

Mheshimiwa Spika,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais ilituma ujumbe wa watu wawili kwenda Mombasa nchini Kenya kufuatilia taarifa za kuokotwa kwa maiti katika fukwe za bahari ya eneo hilo. Jumla ya maiti watano walipatikana na kuzikwa katika maeneo ya Msambweni (1), Shimoni (2) na Wasini (2) chini ya usimamizi wa Balozi Mdogo wa Tanzania aliopo Mombasa. Gharama zilizotumika kwa utafutaji na mazishi zilifidiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia ujumbe huo. Ujumbe huo ulifanya mazungumzo na viongozi na wananchi wa maeneo hayo juu ya kuendelea kushirikiana kutafuta na kutoa taarifa za kupatikana maiti na mizigo ya abiria

3.3. Kukusanya taarifa za watu waliokuwa hawajaonekana kupitia Ofisi za Masheha na Wilaya:

Mheshimiwa Spika,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliziagiza ofisi zote za Wilaya na Shehia kuorodhesha majina ya watu waliokuwa hawajaoneka naambao walisadikiwa kuwemo katika meli hiyo na kuziwasilisha orodha hizo kwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais ili kufanyiwa uhakiki na kupata orodha sahihi kwa ajili ya matumizi na kumbukumbu za baadae. Hadi kufikia tarehe 09 Septemba, 2011 siku ambayo iliwekwa kuwa ni ya mwisho kwa kazi za uorodheshaji, jumla ya watu 2,764 wameripotiwa hawakuonekana ama wakiwa hai au maiti. Hata hivyo, kwa uhakiki wa awali imebainika kwamba baadhi wa watu waliorodheshwa zaidi ya mara moja katika maeneo tofauti Unguja na Pemba.

3.4 Ziara za Viongozi Wakuu wa Kitaifa kutoa mkono wa pole:

Mheshimiwa Spika,
Viongozi Wakuu wa Kitaifa wakifuatana na Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Wabunge, Wawakilishi, Viongozi wa Dini pamoja na Viongozi wengine walifanya ziara za kuzipa pole na kuzifariji familia zilizofiliwa na zilizopotelewa na ndugu zao kwa Wilaya zote zilizoathirika Unguja na Pemba.

Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alianzia kisiwani Pemba tarehe 17 hadi 20 Septemba 2011. Katika ziara hiyo alizifariji jumla ya familia 1026 na kila familia ilipatiwa ubani wa shilingi 100,000/-. Baadae alimalizia ziara hiyo kwa Wilaya zote za Unguja siku ya tarehe 26 Septemba, 2011.Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa Rais alifanya ziara kama hiyo kisiwani Pemba tarehe 13 na 14 Septemba 2011 ambapo alizifariji na kuzipatia ubani jumla ya familia 129.

Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais alianza ziara hiyo Unguja kuanzia tarehe 19 hadi 22 Septemba 2011 na alizifariji jumla ya familia 273, kati ya familia 337 zilizosajiliwa kwa wilaya zote za Unguja na kila familia ilipatiwa ubani wa shilingi 100,000/- . Familia zilizobakia zinaendelea kupatiwa ubani wao kwa utaratibu maalum ulioandaliwa. Kwa ujumla, hadi kufikia sasa familia 1,299 zimefarijiwa na kupatiwa ubani.

Mheshimiwa Spika,
Katika ziara hizo, Viongozi wote hao waliwaomba wananchi kuwa na subira juu ya tukio hilo na kwamba Serikali itaendelea kuwasaidia na iko pamoja nao. Aidha, walielezea kwamba Serikali imeunda Tume ya watu 10 kwa ajili ya kuchunguza chanzo cha ajali hiyo na kutoa mapendekezo kwa Serikali ambapo walisisitiza kwamba mapendekezo yatakayotolewa na Tume hiyo yatafanyiwa kazi sambamba na yale yaliyotolewa na Baraza la Usalama la Taifa.

3.5. Tume ya Uchunguzi ya kuzama kwa meli:

Mheshimiwa Spika
Tarehe 17 Septemba 2011, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alitangaza rasmi kuundwa kwa Tume ya watu 10 ya Uchunguzi wa tukio la kuzama Meli ya M.V. Spice Islanders I. Tume hiyo inaongozwa na Mwenyekiti wake Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar Mhe. Abdulhakim Ameir Issa na sasa Tume hiyo imeshaanza kazi zake rasmi. Tume hiyo itatoa ripoti yake Serikalini siyo zaidi ya mwezi mmoja kuanzia sasa.




3.6. Kuratibu upokeaji wa misaada:

Mheshimiwa Spika,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa inaendelea kupokea misaada ya kifedha na vifaa kutoka kwa watu binafsi, Ofisi za Kibalozi, Mashirika ya Kimataifa, Mashirika ya Umma, Vyama vya Kisiasa, Taasisi za Kidini, Mashirika yasiyo ya Kiserikali na Taasisi mbali mbali za ndani na nje ya nchi.

Hadi kufikia tarehe 11 Oktoba, 2011 jumla ya Shilingi 1,002,775,571/= zimepokelewa na kuingizwa katika akaunti ya Mfuko wa Maafa Zanzibar (Zanzibar Disaster Funds) ilioko Benki ya Watu wa Zanzibar, ambayo imefunguliwa maalum kwa ajili ya michango hiyo. Aidha, vifaa na bidhaa mbalimbali zimepokelewa kwa ajili ya kusaidia shughuli za operesheni. Hivi sasa Serikali inazingatia kwa makini namna ya fedha hizo zitakavyotumika ili kufikia malengo yaliyokusudiwa. Serikali itajadili na kuamua juu ya namna ya kuzitumia fedha hizo.

4.0. GHARAMA ZA UOKOAJI:

Mheshimiwa Spika,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliipatia Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa jumla ya Shilingi Milioni Mia Moja (100,000,000/=) kwa ajili ya kugharamia shughuli za uokoaji ambapo hadi kufikia tarehe 30 Septemba, 2011 fedha zilizotumika ni shilingi 99,984,386/=. Matumizi haya hayahusiani na fedha zilizotolewa kwa ajili ya ubani na uendeshaji wa kazi za Tume ya Uchunguzi.

Mheshimiwa Spika,
Kwa upande wa kutoa ubani kwa ajili ya familia zilizopatwa na msiba huo, Serikali imetoa kiasi cha Shilingi 156,000,000/=.

5.0. TULICHOJIFUNZA KUTOKANA NA TUKIO HILI
(LESSONS LEARNED):

Mheshimiwa Spika,
Kutokana na tukio hili la kuzama kwa meli ya M.V. Spice Islanders I tumeweza kujifunza mambo mbalimbali ambayo ni changamoto kwetu katika kuimarisha kazi na huduma za kukabiliana na maafa nchini. Miongoni mwa mambo hayo kwa mtazamo wa Kamati ya Maafa ni haya yafuatayo: -

1. Umakini na maamuzi sahihi na ya haraka yaliyochukuliwa na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi yameweza kuleta ufanisi mkubwa katika uokoaji ya uokozi na hivyo kupelekea kuokoa maisha ya wananchi wetu wengi.

2. Pamoja na mazingira magumu ya eneo ilikotokea ajali, muitikio wa haraka wa wananchi, hasa wa maeneo ya Nungwi na wa taasisi mbalimbali za kukabiliana na maafa, ikiwemo taasisi za Serikali, vyombo vya ulinzi na usalama, Washirika wa Maendeleo, Sekta Binafsi na Jumuiya za Kiraia umepelekea watu wengi kuweza kuokolewa wakiwa hai pamoja na kupatikana kwa maiti hali ambayo imewezesha maiti wengi kuzikwa na familia zao.

3. Ipo haja ya kuimarisha huduma za mawasiliano wakati wa maafa. Hii inatokana na sababu kwamba wananchi wengi walitumia mtandao wa mawasiliano wa Zantel, na kusababisha ugumu wa mawasiliano kutokana na minara ya kampuni hiyo kuzidiwa na matumizi.

4. Udogo wa sehemu ya kuhifadhia maiti (motuary) ulipelekea maiti wasiotambuliwa na jamaa zao kuzikwa haraka na Serikali.

5. Uhaba wa vifaa vya kisasa vya uokozi pamoja na wataalamu wa uzamiaji (divers) umepelekea zoezi la uokozi kuwa gumu na kuchukua muda.

6. Kukosekana kwa taarifa za uwezo wetu wa ndani wa kukabiliana na maafa ikiwemo uwezo wa vifaa na wataalamu ni changamoto ambayo inapaswa kufanyiwa kazi, na

7. Kukosekana kwa mkakati madhubuti wa kujikinga na maafa ya majini, kivifaa na wataalamu kunapelekea kupata majanga ya ajali za vyombo vya usafiri wa abiria mara kwa mara.

6.0. MIKAKATI YA SERIKALI KATIKA KUKABILIANA NA MAAFA:

Mheshimiwa Spika,
Katika kukabiliana na majanga na maafa mbalimbali yanayoweza kutokea katika nchi yetu, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kutekeleza mikakati mbali mbali ya kukabiliana na maafa, ikiwemo hii ifuatayo:-

1. Kuifanyia mapitio Sheria Nambari 2 ya mwaka 2003 ya kukabiliana na maafa ili iandane na mahitaji na mazingira ya hivi sasa.

2. Kutekeleza kikamilifu Mpango wa Taifa wa Kukabaliana na Maafa pamoja na Mkakati wa Mawasiliano wakati wa Maafa.

3. Kujenga uwezo wa Kitaasisi katika kukabiliana na maafa ikiwa pamoja na upatikanaji wa vifaa na mafunzo kwa wadau mbali mbali.

4. Kutafuta ushauri wa kitaalamu juu ya kuwa na mbinu madhubuti za kujikinga na majanga na maafa mbali mbali yanayoweza kutokea katika nchi yetu pamoja na kufikiria uwezekano wa kuanzisha vituo vya uokozi katika maeneo mbalimbali ya visiwa vya Unguja na Pemba.

5. Kuendelea kutoa elimu ya kukabiliana na maafa kwa jamii na kuimarisha Kamati za Maafa za Shehia, Wilaya na Taifa.

6. Kudhibiti utaratibu wa vyombo vya usafiri vya abiria na mizigo vya baharini na nchi kavu ili kuepusha ajali na upotevu wa maisha na mali za wananchi.

7.0. SHUKRANI:
Mheshimiwa Spika,
Kwa niaba ya Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohammed Shein kwa juhudi zake kubwa alizochukua ili kuhakikisha maisha ya wananchi yanaokolewa. Tunamshukuru kwa maelekezo yake na miongozo aliyotupatia ambayo kwa kiwango kikubwa ilitusaidia kufanikisha kazi za uokozi.

Tunamshukuru Rais, Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuwa nasi kwa hali na mali katika kipindi chote cha maafa haya.

Vile vile, tunamshukuru Makamu wa Kwanza wa Rais Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad kwa kutupatia miongozo ya mara kwa mara katika jitihada za kuokoa maisha ya wananchi na kupunguza athari za maafa yaliyotokea.

Tunatoa shukrani za dhati kwa Baraza la Mapinduzi na Baraza la Usalama la Taifa kwa maelekezo yao juu ya hatua za kuchukuliwa katika kukabiliana na janga hili na majanga yanayoweza kutokea baadae. Shukrani za dhati pia zinatolewa kwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa hatua zao za haraka zilizosaidia kuokoa maisha ya wananchi wengi.

Mheshimiwa Spika,
Shukrani pia zinatolewa kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri majini, angani na nchi kavu kwa jinsi walivyoshirikiana na Serikali katika kulikabili tukio hili. Wananchi wa Nungwi hasa wavuvi na wamiliki wa hoteli na kampuni za kitalii wanapewa shukrani za pekee kwa jinsi walivyoshiriki kikamilifu tokea hatua za awali baada ya kupatikana taarifa za kuzama kwa meli ya Spice Islanders I. Tunawashukuru washirika wa maendeleo na wawakilishi wa nchi marafiki kwa jinsi walivyolichukulia suala hili na kutuunga mkono katika msiba huu mkubwa wa Kitaifa. Vile vile tunazishukuru Taasisi za Kidini hasa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana na Ofisi ya Mufti kwa kusaidia maandalizi ya mazishi ya marehemu wote waliotokana na ajali hiyo.

Tunawashukuru Madaktari na Wauguzi wa Hospitali za Mnazi Mmoja, Kivunge na Bububu Jeshini kwa namna walivyoshirikiana na Kamati. Tunawashukuru Wajumbe wote wa Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa na wafanyakazi wa Idara ya Kukabiliana na Maafa kwa kazi kubwa waliyoifanya kwa kipindi chote toka kutokea kwa janga hili. Tunawashukuru wamiliki wa Vyombo vya Habari na Wanahabari na wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla kwa kupokea tukio hili kwa masikitiko makubwa. Aidha, tunawashukuru wale wote walioweza kuchangia kwa hali na mali katika msiba huu.





7.0. HITIMISHO

Mheshimiwa Spika, Baada ya kutoa maelezo hayo nawaomba Wajumbe wa Baraza lako tukufu waipokee, taarifa hii na kuitafakari.

Mheshimiwa Spika, kwa heshima na taadhima naomba kuwasilisha.


Balozi Seif Ali Iddi
MAKAMU WA PILI WA RAIS,
ZANZIBAR.

OKTOBA, 2011

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.