Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ametoa wito kwa wafanyabiashara, sekta binafsi na sekta za umma kusaidia juhudi za kuendeleza matamasha ya utamaduni nchini ambayo yana umuhimu mkubwa kwa uchumi na maendeleo ya utamaduni wa Zanzibar.
Maalim Seif ametoa wito huo leo huko hoteli ya Zanzibar Beach Resort alipokuwa akifungua kongamano la siku moja la viongozi wa Zanzibar kwa ajili ya utamaduni kukuza uchumi liloandaliwa na Sauti za Busara.
Amesema tamasha la Sauti za Busara linahitaji kusaidiwa ili liendelee kudumu Zanzibar, kwa vile lina mchango mkubwa katika kukuza utalii ambao ni sekta muhimu katika kuimarisha uchumi pamoja na utamaduni wa Wazanzibari.
Makamu wa kwanza wa Rais amesema tamasha hilo pamoja na matamasha mengine ya utamaduni yaliyopo Zanzibar ni muhimu, na kwamba serikali itaendelea kuyaunga mkono ili yawe endelevu.
Amesema serikali ina nia thabiti ya kuendeleza utamaduni wa Zanzibar na taasisi zinazojishughulisha kuendeleza utamaduni, na ndio maana imekuwa ikihamasisha maendeleo ya matamasha mbali mbali likiwemo lile mwa mwaka kogwa.
Amesema utamaduni una nafasi kubwa ya kukuza uchumi wa nchi kwa vile vijana wengine wamekuwa wakijipatia ajira kupitia sanaa za muziki. “Muziki ni ajira na unasaidia sana kuwaunganisha watu wa rika mbali mbali katika jamii” alisema Maalim Seif akinukuu maneno ya aliyekuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Kifi Annan.
Katika hatua nyengine Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar ameelezea haja kwa taasisi mbali mbali ya kijamii na binafsi kuwekeza katika kuendeleza vipaji vya wanamichezo wazalendo ili waweze kuendeleza juhudi zao katika fani hiyo.
Amesema Zanzibar wapo vijana wengi wenye vipaji lakini wamekuwa wakipoteza mwelekeo kutokana na kutonungwa mkono na kushindwa kujiendeleza.
Akiwasilisha mada kwenye kongamano hilo, Mkurugenzi wa Sauti za Busara Zanzibar Bw. Yussuf Mahmoud amesema kuna hatari ya kutoweka kwa tamasha hilo liliodumu kwa miaka kumi hapa Zanzibar, iwapo juhudi za makusudi hazitochukuliwa kuliendeleza.
Mkurugenzi huyo amesema miongoni mwa malengo ya Sauti za Busara ni kukuza na kuendeleza utamaduni na uchumi wa Afrika Mashariki, kuongeza thamani ya muziki wa Afrika ya Mashariki pamoja na kuongeza taaluma na fursa kwa wasanii.
Amefahamisha kuwa matamasha kama haya hayabudi kuendelezwa kwani yamekuwa yakivutia wageni mbali mbali na kukuza sekta ya utalii ambayo ndio tegemeo kuu la uchumi wa Zannzibar kwa sasa, na bila ya kutoa umuhimu wa hali ya juu Zanzibar inaweza kupoteza fursa muhimu kwa maendeleo.
Amesema tamasha la Sauti za busara limekuwa likiitangaza Zanzibar kimataifa na kupelekea kuongezeka kwa wataalii na wageni kila ifikapo msimu wa tamasha hilo na kuongeza ajira na kipato kwa vijana na taifa kwa jumla
Tamasha la Sauti za Busara linalofanyika Februari kila mwaka hapa visiwani linatajwa kuwa moja ya matamasha matano yanayoongoza barani Afrika katika kuendeleza utamaduni, muziki, vipindi, taaluma na kukuza urafiki.
Hassan Hamad (OMKR)

No comments:
Post a Comment