Habari za Punde

UJUMBE WA CHAMA CHA KIKOMUNISTI CHA CHINA KUTEMBELEA ZANZIBAR

Na Mwandishi Maalum

UJUMBE wa Chama Tawala cha Kikomunisti (CPC) cha China, unatarajia kuwasili mjini Zanzibar leo kwa ziara ya kisiasa ya siku moja kwa mwaliko wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, ilisema ugeni huo utakuwa na watu 26 utawasili Zanzibar majira ya asubuhi.


Alisema ujumbe wa chama cha CPC utaongozwa na Mjumbe wa Kamati Kuu anayeshughulikia dawati la siasa katika Idara ya Uenezi ya chama hicho, Liu Yunshan.

Vuai alisema lengo kuu la ziara hiyo, ni kukuza na kudumisha uhusiano wa muda mrefu baina ya CCM na CPC pamoja na kubadilishana mawazo juu ya utendaji wa kazi.

Chama Cha Mapinduzi na CPC ni vyama vya kidugu vyenye mahusiano ya kihistoria tokea enzi za uhai wa uongozi wa Mwenyekiti Mao Thentung kwa upande wa CPC na Mwalilim Julius Kambarage Nyerere kwa CCM.

Aidha Naibu huyo Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar alifafanua kuwa ujumbe huo utapata fursa ya kukutana na Mjumbe wa Kamati Kuu ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi kabla ya kuzungumza na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk. Amani Abeid Karume.

Hitimisho la ziara ya ujumbe huo wa CPC Visiwani humu utakamilika baada ya kutembelaa maeneo mbali mbali ya kihistoria ya Zanzibar ikiwemo Mji Mkongwe pamoja na Palace Museum mjini Unguja.

Ugeni huo unatarajia kuondoka Zanzibar majira ya jioni kuelekea nchini Zimbabwe kuendelea na ziara kama hiyo nchini humo

Wakati huohuo ujumbe wa wafanyabiashara kutoka nchini Singapore unatarajiwa kuwasili Zanzibar hapo kesho, ambapo unatarajiwa kuwa na mazungumzo na viongozi wa wizara ya Biashara ,Viwanda na Masoko.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.