Habari za Punde

KILA MMOJA AHAMASISHE CHANJO KWA WATOTO - DUNI

Na Juma Masoud

WAZIRI wa Afya, Juma Duni Haji ameeleza kusikitishwa na watu wanaoendelea kukwepa kuwapeleka watoto kwenye chanjo kuwakinga na maradhi mbali ikiwemo, Polio, Surua na magonjwa mengine yanayowasibu zaidi watoto.

Alisema kitendo cha kumkosesha mtoto chanjo ni cha kumkatli mtoto kwani hiyo ni moja ya haki zake za kimsingi ili kumuepusha na maradhi mbali mbali yanayoweza kumpata tokea akiwa mdogo.


Duni aliiambia kamati ya kitaifa ya chanjo iliyokutana Wizara ya afya jana kwamba haoni sababu ya mzee au mlezi kumkosesha chanjo mtoto, akisisitiza kwamba kinga ni bora kuliko tiba.

Kamati hiyo ya kitaifa ya chanjo inyowajumuisha viongozi wa dini wakuu wa Mikoa, imekuwa ikifanyika tokea Oktoba mwaka huu kwa kushiriki katika maandalizi ya chanjo ya kitaifa itakayofanyika jumamosi ya Novemba 12 hadi Novemba 14.

Waziri huyo wa Afya ambaye atazindua chanjo kitaifa huko Mwambe Pemba kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, amehimiza kila mtu kubeba ujumbe wa chanjo na kuufikisha kwa mwengine.

Alisema jamii inapaswa kujilaumu kwa kutolipa uhimu mkubwa suala la afya zao kwa kutopendelea kujichunguza afya hadi anapopatwa na maradhi, kutokana na kushindwa kujikinga.

Hata hivyo, Waziri Juma Duni aliishauri kamati hiyo kupitia wataalamu wake kuangalia kasoro zozote zilizopo ili kufanikisha kampeni hiyo ya siku tatu itakayoanza kesho.

Wajumbe wa kamati hiyo wakiwemo wakuu wa mikoa ya Kaskazini Unguja, Pembe Juma, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Abdulla Mwinyi Khamis na mwakilishi waMkoa wa Kusini Unguja walishauri mabadiliko mbali mbali katika chanjo itakayofuata ili kuhakikisha kwamba kila mtoto anapatiwa chanjo inayofanyika nchi nzima, Bara na Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.