Na Salum Vuai, Maelezo
ZANZIBAR itaanza kampeni za kuwania ubingwa wa Chalenji kwa kupambana na timu ya taifa ya Uganda, The Cranes’ kwenye uwanja wa taifa Dar es Salaam Novemba 25.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa jana na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), mchezo huo utachezwa saa 10:00 jioni baada ya ule wa ufunguzi utakaozikutanisha timu za Burundi na
Somalia, michezo yote ikiwa ya kundi B.
Ratiba hiyo inaonesha kuwa, wenyeji wa michuano hiyo inayodhaminiwa na Kampuni ya Bia Serengeti timu ya Kilimanjaro Stars, watatupa karata ya kwanza Novemba 26, kwa kuikaribisha Amavubi ya Rwanda, ukiwa mchezo pekee kwa siku hiyo.
Zanzibar, inayonolewa na Muingereza Stewart John Hall, itakuwa kibaruani tena Novemba 27, itakapotiana mikononi na Burundi, huku waalikwa Namibia walioko kundi A, watapimana nguvu na Djibouti.
Mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi kwa Zanzibar Heroes, utachezwa Disemba 1, mwaka huu, ambapo watamaliza ngwe kwa kuivaa timu ya Somalia wakati wa saa nane mchana, huku mechi nyengine ya kundi hilo la B, utazikutanisha timu za Uganda na Burundi.
Mechi zote hizo zitachezwa katika uwanja wa taifa, ukiondoa ule wa kundi B kati ya Somalia na Uganda, ambao ndio pekee utakaotimua vumbi kwenye uwanja wa Azam FC ulioko Chamazi.
Michezo ya robo fainali ya ngarambe hizo, itapigwa Disemba 5 na 6, ambapo kila siku kutakuwa na mechi mbili, na ile ya nusu fainali imepangwa kuchezwa Disemba 8.
Fainali ya michuano hiyo inatarajiwa kuwa Disemba 10, ikitanguliwa na mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu.
Bingwa wa mashindano hayo ni Kilimanjaro Stars, ambao iliutwaa katika michuano iliyopita jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa mwaka huu.
Kikosi cha Zanzibar Heroes kimepiga kambi ya wiki mbili nchini Misri, kujiweka vyema kabla kutia mguu katika patashika hiyo.
No comments:
Post a Comment