CHAMA Cha Mapinduzi kisema bila ya uimara wa chama hicho na viongozi wake, taifa kuendelea kuwa na amani, mshikamano na maendeleo ndoto hizo zinaweza kutoweka.
Katibu wa Kamati Maalum wa Itikadi na Uenezi, Issa Haji Gavu alieleza hayo katika mkutano na wake na wajumbe wa kamati za siasa za matawi, wadi na Jimbo la Chwaka, wilaya ya Kati, Unguja.
Gavu ambaye ni Mwakilishi wa Jimbo hilo na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Miundombinu, alisema CCM ndicho chama pekee kinatambua shida zinazowakabili wananchi na serikali zake zimekuwa mstari wa mbele kuzipatia ufumbuzi shida hizo kila hali inavyoruhusu.
Alisema misingi ya amani iliyopo Tanzania ni dhamana kuu inayosimamiwa na kulindwa kwa uaminifu na serikali za CCM, hivyo bila ya CCM imara nchi inaweza kujikuta ikiyumbishwa na wapenda madaraka.
Alifahamisha kuwa wakati umefika kwa viongozi na wanachama wa CCM kujiamini na kujenga ujasiri wa kuyaelezea bayana yale yanayofanikishwa na serikali zao bila ya woga wala aibu.
Katibu huyo, aliwataka wana CCM kutambua umuhimu wa kukutana, kujadiliana na kupanga mambo yao ya kimaendeleo ya nchi kupitia vikao vyao vya kikatiba.
Aidha Gavu aliwahimiza viongozi hao wa Jimbo la Chwaka, kujenga moyo wa kujituma na kufanya kazi kwa bidii, kushughulikia kero za kijamii pamoja na matatizo yaliopo ndani ya maeneo kwa wakati muafaka.
Wakati huo huo, Chama Cha Mapinduzi kimesema viongozi wa CCM wana wajibu wa kujivunia mafanikio yanayotokana na utekelezaji wa sera zilizomo kwenye ilani yake ya uchaguzi.
Katibu wa CCM Mkoa Kusini Unguja, Shija Othman Shija alibainisha hayo katika mkutano wake na wajumbe wa kamati za Siasa za Jimbo la Chwaka, wilaya ya Kusini Unguja.
Shija alisema si jambo la busara kwa viongozi na wanachama wa CCM kupata kigugumizi katika kuyaeleza mambo yote mazuri yaliyotekelezwa na yanayoendelea kutekelezwa na serikali zao kwa maslahi ya jamii.
Alisema chini ya mfumo wa vyama vingi vya siasa, ushindani wa kisiasa huongezeka hivyo iwe ni mwiko kwa viongozi kujisahau na kwamba wanapasa kuyanadi kwa nguvu zote mafanikio yote yanayofanikishwa.
Akifafanua zaidi Shija alisema serikali za CCM tokea ziwe madarakani zimekuwa zikifanikisha mambo ya msingi hasa katika kuimarisha huduma za jamii na kushamirisha maendeleo ya kisekta.
Aidha Katibu huyo wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja, alisema ikiwa viongozi na wanachama wa CCM wataamua kuzubaa kwa kutoyatangaza yanayotekelezwa watatoa mwanya kwa wapinzani kuteka nyara mafanikio hayo na kuyatangaza kuwa ni yao.
No comments:
Post a Comment