Na Mwajuma Juma
TIMU za Taifa za netiboli Tanzania kwa wachezaji wanawake na wanaume, zinaendelea vyema na mazoezi zikiwa kambini kwa ajili ya kujiandaa na mashindano ya Kombe la Mapinduzi, yatakayoshirikisha nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Mashindano hayo yaliyopangwa kuanza Januari 6, mwakani, yatashirikisha nchi sita ambazo ni Uganda, Kenya, Zimbabwe, Zambia, Msumbiji na wenyeji Tanzania.
Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Netiboli Zanzibar (CHANEZA) Rahima Bakari, amesema kuwa wachezaji wa timu hizo wanaonolewa na Kocha Mkuu Marry Protas akisaidiwa na Restuta Lazaro, wameanza kambi tangu Disemba 25 mwaka huu, huko katika hoteli ya uwanja wa Amaan mjini hapa.
Rahima alisema timu hizo zinaundwa na wachezaji 12 kwa wanaume na 14 kwa ile ya wanawake, ambapo kwa upande wa kinadada, tayari wachezaji sita wamesharipoti, huku wenzao wa Tanzania Bara, wakitarajiwa
kuwasili wakati wowote.
Aliwataja wachezaji wa timu hiyo kuwa ni Pili Peter, Miza Nyange, Margareth Constantine, Mainda Rogers, Siwa Juma na Asha Ibrahim wote kutoka klabu za Zanzibar, na wale wa Bara ni Mwanaidi Hassan, Neila
Nyangaisiye, Evolia Kizinja, Doris Mbunda Lulu Joseph, Faraja Malaki, Jackline Sheneza na Teya Pascari.
Timu ya wanaume inaundwa na Abbas Muhidini, Mohammed Kassim, Habib Kassim, Mohammed Uwesu, Muhidini Mussa na Said Ali, Yahya Anania, Abdallah Mohammed, Abdulhakim Khamis, Ramadhan Amour, Mohammed Juma na Silima Seif, bila kutaja wale wanaotoka Bara.
Wakati huohuo, vifaa vitakavyotumika kwa ajili ya mashindano ya soka na netiboli kuwania Kombe la Mapinduzi, vimewasili mjini Zanzibar, ambapo Mwenyekiti wa kamati ya michuano hiyo Mohammed Raza alivikabidhi kwa kamati, ambapo miongoni mwa vifaa hivyo ni vikombe, medali na fulana.
Akizungumza katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Bahari hoteli ya Bwawani, Raza vifaa hivyo vina thamani ya shilingi milioni 10, na kwamba vyengine vitawasili wakati wowote wiki hii.
No comments:
Post a Comment