Na Haroub Hussein
KAMATI ya mashindano ya kuwania Kombe la Mapinduzi kwa upande wa mpira wa miguu, imeweka hadharani bei za tiketi kwa mashabiki watakaokwenda uwanjani kushuhudia ngarambe hizo zinazotarajiwa kuanza Januari 2, mwakani.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Mshika Fedha wa kamati hiyo Amani Ibrahim Makungu, kutakuwa na bei tafauti kwa mechi za jioni na usiku.
Akizitaja bei hizo, Makungu alisema watazamaji watakaopenda kukaa jukwaa kuu (VIP), watalazimika kulipa shilingi 5,000 jioni, ambapo wakati wa usiku watakamua mifuko yao kutoa shilingi 10,000.
Aidha alisema majukwaa ya pembeni mwa VIP, tiketi zitauzwa kwa shilingi 2,000 jioni, na 3,000 kwa mapambano ya usiku, ambapo majukwaa ya Urusi, Orbit na jukwaa la saa, tiketi za jioni zitagharimu shilingi
1,000 na zile za usiku itakuwa shilingi 2,000.
Wakati huo huo, Makungu amefahamisha kuwa, Rais mstaafu wa awamu ya sita Dk. Amani Abeid Karume, ndiye atakayekuwa mgeni rasmi katika mechi ya ufunguzi itakayozipambanisha Yanga kutoka Dar es Salaam na Mafunzo itakayopigwa wakati wa saa 2:00 usiku.
Pamoja na mashindano hayo kuanza kwa mechi kati ya Azam FC na Kikwajuni mnamo saa 10:00 jioni, Makungu alisema mechi hiyo ya usiku ndiyo itakayokuwa ya uzinduzi wa patashika hiyo inayofanyika
kuadhimisha miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12,1964.
No comments:
Post a Comment