NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo (WHUUM), Bihindi Hamad Khamis, amesema Serikali inathamini sana mchango wa wasanii katika kukuza na kuendeleza utamaduni na ndio sababu iko mbioni kujenga Studio ya kisasa ya kurekodia.
Amesema hayo jana katia ukumbi wa Bait el Yamin Malindi, katika kilele cha mahafali ya nne ya Mafunzo ya ‘kusarifu na kutengeneza filamu na matumizi ya Komputa’yalioendeshwa na taasisi ya kiraia (NGO) ya ZANZIBITS.
Jumla ya wanafunzi 18 wamehitimu mafunzo hayo ya mwaka mmoja, yenye lengo la kuwaandaa vijana kukabiliana na hali ya maendeleo ya Sayansi na teknolojia, sambamba na kuwajengea uwezo wa kujiajiri.
Akimuwakilisha Waziri wa Wizara hiyo, alisema Serikali iko mbioni kujenga Studio ya kisasa ya kurekodia, ili kuwawezesha wasanii wa Zanzibar kurekodi kazi zao bila usumbufu na kuepuka gharama za ziada.
Aliwataka vijana hao kuienzi na kuitumia vyema taaluma waliyoipata kwa maslahi ya jamii na kuepuka utengenezaji wa filamu zisizozingatia maadili na kuipotosha jamii.
Alisema Zanzibar hivi sasa inakabiliwa na changamoto kubwa ya kuzagaa kwa filamu na sanaa nyingine zisizozingatia maadili, hivyo kutaka juhudi zichukuiliwe kukabiliana na hali hiyo.
‘Hivi sasa kuna wimbi la filamu zisizoendana na maadili yetu na nyingine zinatengenezwa na Watanzania, kwa kweli huu ni msiba mkubwa, sote kwa pamoja tuupige vita na kulaani’ alisema.
Alisema Wizara yake kupitia Bodi ya Sensa na Filamu, inaandaa mikakati kabambe itakayowezesha kuwanasa watengenezaji, wasambazaji na waoneshaji wa filamu na sanaa zinazoathiri mila, silka na utamaduni wa Wazanzibari.
Alieleza Wizara yake inalaenga kushirikiana na taasisi mbali mbali za kijamii katika kuendeleza utamaduni, hivyo aliwataka vijana hao kuitumia kimailifu kupata ushauri, maelekezo na miongozo itakayowawezesha kufanikisha malengo yao.
Aidha aliwataka vijana hao kuwa tayari kukabiliana na changamoto ijayo juu ya mabadiliko ya teknolojia, wakati huu Dunia ikijiandaa kuhama kutoka mfumo wa matangazo ya Analojia kuelekea Digital, na kuwahakikishia kuwa Serikali imejipanga vyema kuhusu jambo hilo.
Katika hatua nyingine Bihindi aliwataka vijana hao kutobweteka na kiwango cha elimu walichofikia na badala yake aliwashauri kujipanga upya na kutafuta fursa nyengine za kujifunza, kwa kigezo kuwa elimu inakuwa kila kukicha.
Mapema Mratibu wa taasisi hiyo Salama Haji Ali, alisema taasisi hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa ya kujiendesha baada ya mdhamini wake Guy Mullenf ‘Mussa’ raia wa Uholanzi, kumaliza mkataba wake.
No comments:
Post a Comment