Na Mwajuma Juma
TIMU ya soka ya Zimamoto imefanikiwa kuondoka na pointi tatu muhimu katika mchezo wa Ligi Kuu ya Seagull baada ya kuifunga Mundu ya Nungwi magoli 3-2.
Pambano hilo lilipigwa kwenye uwanja wa Mao Dzedong ambapo sasa Zimamoto imefikisha pointi nne sawa na Mafunzo ilishuka dimbani juzi.
Katika mchezo huo ambao haukupata watazamaji wengi, mchezaji wa Mundu, Haji Ameir, alitolewa nje kwa kadi nyekundu na muamuzi, Ramadhan Ibada Kibo, baada ya kumchezea rafu Khatib Said katika dakika ya 81.
Zimamoto ndio iliyotangulia kupata goli katika mchezo huo kupitia kwa mchezaji wake, Hakim Khamis, kwenye dakika ya 38, ambalo liliweza kudumu hadi mapumziko.
Kuanza kwa kipindi cha pili, Mundu walijaribu kujirekebisha makosa yao na kujipanga upya na ndipo walipofanikiwa kusawazisha goli hilo katika dakika ya 66 kupitia kwaao William Sylvesta.
Miamba hiyo iliyokuwa ikishambuliana kwa zamu iliweza kuendeleza mashambulizi hayo kila dakika ambapo Zimamoto ilipata goli la pili katika dakika ya 70, lilofungwa na Hamid Mgeni wakati goli la tatu lilifungwa tena na Hakim Khamis dakika tatu baadae.
Goli la pili la Mundu liliwekwa kimiani na mchezaji Himid Mkasi katika dakika ya 88 ya mchezo huo.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena leo kwa mchezo utakaowakutanisha Kikwajuni na Miembeni SC huku katika uwanja wa Gombani, Pemba Chipukizi itakwaruzana na Miembeni United.
No comments:
Post a Comment