Na Haji Nassor, Pemba
WIKI kadhaa baada ya kupewa darsa na Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ), vyama vya mchezo wa Baiskeli na Karate vya Wilaya ya Chake Chake vimeanza kutafuta njia za kujiendesha badala.
Katika ziara yake kisiwani Pemba hivi karibuni, Mwenyekiti wa BTMZ Sharifa Khamis Salim 'Sherry', aliviasa vyama mbalimbali vya michezo kusaka njia za kujitafutia mapato ya kuendeshea shughuli zao, badala
ya kukunja mikono na kusubiri ruzuku kutoka serikalini.
Kufuatia ushauri huo, vyama vya Baiskeli na Karate, vilifanya kikao cha pamoja wiki iliyopita na uongozi wa BTMZ Wilaya ya Chake Chake chini ya Katibu wa baraza hilo Ali Juma Sufi, na kukubaliana kufanya
maonesho mara mbili kila mwezi katika uwanja wa Gombani.
Katibu huyo wa BTMZ Chake Chake, ameliambia gazeti hili kuwa, kupitia maonesho hayo, vyama hivyo vitaweza kuingiza angalau fedha kidogo.
Alifahamisha kuwa, kwa vile katika maonesho hayo kutakuwa na kiingilio kati ya shilingi 500 na 1000, vyama vitaweza kujiwekea akiba, na pale vinapokuwa na safari hasa za ghafla, zitaweza kuwasaidia na kuondokana
na tabia ya omba omba kwa asilimia 100.
"Pamoja na kupata fedha, lakini maonesho hayo yatawasaidia hata wanamichezo fiti, na kuwa tayari kushiriki mashindano wakati wowote", alieleza Sufi.
Nao viongozi wa vyama hivyo, walisema mpango wa kutegemea ruzuku pekee kutoka serikalini kwa sasa hauna nafasi kubwa, maana wakati mwengine hujitokeza ukosefu wa fedha japo chache na kushindwa kushiriki hata mashindano yanayohitaji gharama ndogo.
Walifahamisha kuwa, wazo hilo ni zuri na wanaliunga mkono, pamoja na kuahidi kuwashajiisha wanachama wao kushiriki kwenye maonesho hayo kuvipa uhai vyama na wanachama wao.
No comments:
Post a Comment