Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza baada ya kufungua mradi wa maji wa Kiuyu na Maziwang’ombe katika Wilaya ya Micheweni.Wengine kutoka kulia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi Said Ali Mbarouk na Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Ali Juma Shamuhuna..
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akifungua mradi wa maji wa Kiuyu na Maziwang’ombe, ikiwa ni shamrashamra za kuadhimisha miaka 48 ya Mapinduzi.
(Picha, Salmin Said OMKR) Hassan Hamad (OMKR)
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema kuimarika kwa miundombinu katika Wilaya ya Micheweni kutalifanya eneo hilo kutimiza azma ya serikali ya kulifanya kuwa eneo huru la kiuchumi.
Amesema wawekezaji watavutiwa zaidi kuwekeza vitega uchumi vyao ikiwa watahakikishiwa upatikanaji wa huduma muhimu zikiwemo maji, barabara na umeme.
Makamu wa Kwanza wa Rais alieleza hayo jana huko Micheweni Pemba baada ya kufungua mradi wa maji wa Kiuyu na Maziwang’ombe, ikiwa ni katika shamrashamra za maadhimisho ya miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Maalim Seif ameitaka Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati kuutunza mradi huo na kuhakikisha kuwa huduma hiyo inawafikia wananchi kwa wakati wote.
Kwa upande wake Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Ali Juma Shamuhuna amesema kufunguliwa kwa mradi huo katika Wilaya ya Micheweni kunathibitisha nia ya serikali kuwakomboa wananchi wa maeneo yote ya Unguja na Pemba.
Mradi huo uliosimamiwa na kujengwa na mafundi wazalendo wa Mamlaka ya maji Zanzibar ZAWA kwa kushirikiana na mafundi wa Idara ya Ujenzi umetekelezwa kwa pamoja kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mashirika ya Umoja wa Mataifa, na umegharimu zaidi ya shilingi milioni mia tano.
Wakati huo huo Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad ameitembelea na kuifariji familia iliyofikwa na msiba mkubwa uliotokana na kula kasa katika kijiji cha Tumbe Wilaya ya Micheweni.
Katika msiba huo watu wanane wakiwemo saba wa familia moja walifariki dunia hivi karibuni, wengi wao wakiwa ni watoto.
Ameitaka familia hiyo kuwa na subra katika kipindi hiki kigumu cha msiba na kuwaombea marehemu makazi mema Peponi.
No comments:
Post a Comment