Na Masanja Mabula, Pemba
JESHI la Polisi Mkoa wa Kasakazini Pemba, limemfikisha mahakamani Seif Juma Seif (52) mkaazi wa Chaleni Msuka, akikabiliwa na shitaka la kupatikana na majani makavu yanayosadikiwa kuwa ni bangi mafurushi 62.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka iliyowasilishwa mahakamani hapo na mwendesha mashitaka wa Polisi, Salum Khelef mbele ya hakimu wa mahakama hiyo Omar Suleiman Khamis wa mahakama ya mwanzo Wete,
mshitakiwa huyo alikamatwa Januari 3 majira ya saa 4.17 huko Chaleni wilaya ya Micheweni.
Mwendesha mashitaka huyo aliieleza mahakama kuwa mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 16 (1) (a) sheria No 9/ 2009 sheria ya kuzuia uingizaji na utumiaji wa dawa za kulevya sheria za serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Hata hivyo mtuhumiwa huyo hakutakiwa kujibu lolote kutokana na kesi hiyo kupaswa kusikilizwa katika mahakama ya Mkoa na mtuhumiwa huyo yuko nje kwa dhamana hadi Januaria 25 kesi yake itakapokuja kutajwa tena katika mahakama ya Mkoa.
Mtuhumiwa yuko nje baada ya kutimiza masharti ya dhamana ambapo alitakiwa kujidhamini mwenyewe kwa shilingi 500000 za maandishi pamoja na wadhamini 3 kila mmoja shilingi 300,000 za maandishi.
Mtuhumiwa huyo alikamatwa na jeshi la polisi Mkoa huo kwa msaada mkubwa kutoka kwa Polisi Jamii na wananchi ambao walitoa taarifa baada ya kubaini kuingizwa mazigo wa bangi katika kijiji chao.
Baada ya kupokea taarifa hizo , jeshila polisi liliweka mtego ambao ulifanikisha kumtia mikononi mtuhumiwa huyo , ambapo pia alijaribu kuwashawishi askari kwa kutaka kuwapa rushwa ya shilingi laki 9 ili wamuachie.
No comments:
Post a Comment