Na Donisya Thomas
NIDHAMU, mshikamano na ari ya kujituma, ndio siri ya mafanikio ya klabu ya Azam FC iliyomudu kutwaa ubingwa wa mashindano ya Mapinduzi mwaka huu.
Nahodha wa timu hiyo Aggrey Morris, amesema pia mshikamano wa viongozi pamoja na maelekezo ya kocha, nako kumechangia kwa kiasi kikubwa kuiwezesha klabu hiyo kubeba kikombe cha kwanza tangu kuanzishwa kwake.
Morris alifahamisha kuwa, baada ya Azam FC kupata nafasi ya kushiriki michuano hiyo, kocha wao Muingereza Stewart John Hall, aliwataka kujituma kwa kiwango cha juu ili kuwavutia mashabiki na hata waandaaji wasijutie uamuzi wa kuialika klabu hiyo tajiri hapa nchini.
"Tunamshukuru Mungu, kile tulichokusudia kukifanya na kuwaahidi wapenzi wetu, tumefanikiwa sasa tunajipanga zaidi kuhakikisha tunatwaa ubingwa wa Tanzania Bara, na hilo linawezekana kutokana na ari na
uwezo tulionao", alisema nyota huyo wa Zanzibar Heroes na Taifa Stars.
Aidha alisema kiwango kizuri walichoonesha katika mashindano hayo, si uchawi bali kilitokana na kujituma kwa mazoezi ya nguvu wanayopewa na mwalimu wao, huku nao wakijengwa kitimu, umoja na mshikamano mambo aliyoyataja kuwa ndio siri ya mafanikio yao.
Aidha mlinzi huyo wa kati anayetarajia kufunga ndoa mwezi Julai mwaka huu, alisema ana imani kubwa kuwa timu hiyo itafanya vizuri katika mashindano tafauti itakayoshiriki na kufika mbali kutokana na umoja
wao, huku akiisifia kuwa ndio timu pekee nchini inayoendeshwa kisayansi bila ya migogoro.
Alizishauri klabu nyengine kuiga mfano wa Azam kwa kujiepusha na migogoro ya mara kwa mara, kama zinataka kupata ufanisi na maendeleo ya muda mrefu.
Nahodha huyo aliyejipatia sifa nyingi kutokana na uchezaji wake, alikuwa mlinzi wa kutegemewa na mabingwa wa soka Zanzibar, Mafunzo, kabla kunasa katika himaya ya matajiri wa SSB (Said Salim Bakhresa) msimu uliopita
No comments:
Post a Comment