Habari za Punde

ZFA Yatakiwa Iwasikilize Wadau

Na Mwajuma Juma

CHAMA cha Soka Zanzibar (ZFA), kimeombwa kuzingatia mawazo na ushauri unaotolewa na wataalamu wa soka visiwani humu, ili kuleta ufanisi katika mikakati ya kuinua kiwango cha soka la Zanzibar.

Ushauri huo umetolewa na mmoja wa wadau wa mchezo wa mpira wa miguu hapa Zanzibar Rashid Omar 'Lato', ambaye alisema visiwa hivyo vimejaaliwa kuwa na wataalamu wengi wazoefu katika uendeshaji soka,
lakini wanapotoa ushauri wao hawasikilizwi.


"Kutokana na hali hiyo, imekuwa vigumu kuendeleza mpira hapa nchini, na sasa umeanza kufa taratibu, hali inayoashiria Zanzibar kufutika katika ramani ya soka kama uongozi wa ZFA hautabadilika", alifafanua.

Alitolea mfano wa wachezaji wa zamani walioiletea sifa Zanzibar ambao wamejikusanya na kuunda timu yao 'Wazee Sports', na kusema kama watashirikishwa kikamilifu, wana uwezo mkubwa kuleta mageuzi na
kuirejeshea Zanzibar hadhi iliyokuwa nayo kisoka.

Katika kipindi cha takriban miongo miwili, Zanzibar imeshuhudiwa ikiporomoka katika mchezo wa mpira wa miguu, tafauti na ilivyokuwa kwenye miaka ya 70,80 na 90, ambapo pia kwa mara ya kwanza, iliandika
historia kwa kutwaa ubingwa wa Chalenji mwaka 1995, katika mashindano yaliyofanyika nchini Uganda.

Tatizo kubwa linalotajwa kuchangia hali hiyo, ni uongozi wa ZFA kukosa dhamira na mipango madhubuti kiasi cha kuikosesha mvuto ligi kuu ya Zanzibar, ambayo mwaka 2011/12, kumeshuhudiwa ubabaishaji mkubwa katika suala la udhamini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.