Katika Sekta za Maendeleo
NA Rajab Mkasaba, Ikulu
SERIKALI ya Norway imeahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya afya na kupongeza uendelezaji wa amani na utulivu nchini ambavyo ndio chachu ya maendeleo.
Waziri wa Afya wa Norway Mhe. Mama Anne Grestestrom Erichsen, aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu mjini Zanzibar.
Katika maelezo yake Waziri Erichsen alimueleza Dk. Shein kuwa Norway inajivunia uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati yake na Zanzibar ambao ni wa muda mrefu hatua ambayo itaimarika kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta zake za maendeleo ikiwemo sekta ya afya.
Alieleza kuwa kabla ya mashirikiano na mahusiano katika sekta ya afya, tayari Norway ilikuwa na uhusiano mzuri na Zanzibar, hatua ambayo ilipelekea kusaidia kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo barabara na umeme.
Waziri Erichsen alieleza kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ambayo Norway iliiunga mkono Zanzibar ni pamoja na Mradi wa umeme kutoka Tanga kwenda kisiwani Pemba sanjari na mradi wa usambazaji wa umeme vijijini.
Kutokana na hatua hizo Waziri Erichsen alieleza kuwa amefarajika na uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo tokea wakati huo hadi hivi leo na ndipo nchi yake ikapanua zaidi mashirikiano kwenye sekta ya afya ambayo kabla ya hapo iliwezwa kuungwa mkono na nchi hiyo kupitia ujenzi wa barabara na usambazaji umeme.
Aidha, Waziri huyo ambayo alifika Ikulu mjini Zanzibar akiwa na ujumbe wake alimueleza Dk. Shein kuwa Norway imeona jambo la busara la kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya ambapo tayari mchakato wa mashirikiano katika sekta hiyo umeanza rasmi.
Alieleza kuwa kujengwa kwa nyumba ya Madaktari kutoka Norway huko Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar ni hatua moja kubwa ya ushirikiano ambao umeimarika zaidi kati ya Hospitali ya MnaziMmoja na Hospitali ya Haukland ya Norway.
Pamoja na hayo, Waziri Erichsen alitoa pongezi kwa uongozi wa Dk. Shein kwa kuendeleza amani, utulivu na mshikamano nchini hali ambayo aliisema kuwa ni chachu ya maendeleo endelevu hapa Zanzibar.
Nae Dk. Shein kwa uoande wake alitoa pongezi kwa Serikali ya Norway kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo bila ya kusahau mchango wake mkubwa katika kuimarisha huduma za umeme na barabara hapa Zanzibar.
Dk. Shein alieleza kuwa mbali ya Serikali ya Norway kusaidia mradi mkubwa wa umeme kutoka Tanga hadi Pemba sanjari na usambazaji wa umeme vijijini pia, ilisaidia katika kuimarisha huduma za benki ya damu hapa Zanzibar.
Aidha, Dk. Shein alitoa shukurani zake kwa Norway pamoja na uongozi wa hospitali ya Haukland kwa utekelezaji wa mazungumzo ya msaada wa huduma za maradhi ya figo, saratani na figo ambapo mtaalamu wa maradihi ya figo anatarajiwa kufika nchini hivi karibuni kwa ajili ya mpango wa utekelezaji.
Dk. Shein alimueleza Waziri huyo kuwa utekelezaji wa Mkataba wa Maelewano juu ya mashirikiano kati ya hospitali ya ManaziMmoja na Hospitali ya Chuo Kikuu ya Haukland utasaidia katika kuiamrisha sekta ya afya hapa Zanzibar.
Alieleza kuwa azma ya Chuo cha Sayansi ya Afya cha Zanzibar ya kuanzisha mafunzo ya uhandisi wa vifaa vya hospitali utasaidia katika kuimarisha ubora wa utoaji wa huduma za afya na kutokana na uungwaji mkono na chuo kikuu hicho cha Norway kutasaidia kufikia malengo yaliokusudiwa.
Rajab Mkasaba,Ikulu Zanzibar
No comments:
Post a Comment