Habari za Punde

Serikali Yaombwa Kuunga Mkono Jitihada za NGOs

Na Asya Hassan

KATIBU wa Jumuia ya Mazingira ya Vijana ‘WAPE Cooperative’ ya Tomondo Yohana Peter Martin, amesema upo umuhimu kwa serikali kuzisaidia jumuia zisizo za kiserikali ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Katibu huyo alieleza hayo hivi karibuni huko ofisini kwake alipokua akizungumza na gazeti hili Tomondo, wilaya ya Magharibi.


Martin alisema suala la uharibifu wa mazingira sio janga la Zanzibar pekee bali ni la kiduni hivyo, serikali kuziunga mkono jumuia hizo kutasaidia kupunguza athari za kimazingira.

Alisema jumuia yake imejikita katika utoaji wa elimu juu ya athari za mazingira pamoja na kuifunza jamii kuachana na uharibifu wa mazinfgira kwani athari zake zimekuwa zikisababisha majanga ambayo huwakumba
wananchi.

“Tunaweza kumaliza matatizo ya uchafu wa mazingira kwa kila madu kuwajibika ipaswavyo katika eneo lake”,alisema Katibu huyo.

Alifahamisha kuwa wameamua kuanzisha jumuia hiyo inayojishughulisha na usafi wa mazingira kutokana na kuona umuhimu wa kuifanya shughuli hiyo kwa ustawi bora wa jamii.

Alisema viongozi kadhaa wa serikali akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kukerwa na tabia ya uchafu mijini ambapo jumuia hiyo itasaidia kusafisha mazingira.

Matin alisema kuwa jumuia yao inafanya kazi mbalimbali kama vile kuwahamasisha vijana kufanya usafi katika shehia yao na kupanda miti pembezoni mwa barabara kuanzia Mazizini hadi Fumba.

Hata hivyo alifahamisha kuwa jumuia yao inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo ukosefu wa misaada kutoka kwa wafadhili na serikali.

Nae mwanachama katika jumuia hiyo Siajab Khamis Ali alisema kuwa jumuia hiyo imejitolea katika kuhakikisha inadhibiti hali ya usafi wa eneo lao na kupanda miti kwa lengo la kuzuia uharibifu wa mazingira.

Hata hivyo aliwataka viongozi kuwawezesha katika jumuia yao kwani tayari jumuia hiyo imesha jitolea kwa kuhifadhi mazingira. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.