Habari za Punde

Simba, Azam Patachimbika

Ni vita kati ya kocha Muingerzea, Mserbia

Na Salum Vuai, Maelezo

MAKOCHA wawili wa kigeni Muingereza Stewart John Hall na Milovan Sircovic kutoka Serbia, leo watakuwa katika mpambano mgumu kudhihirisha nani zaidi kati yao, wakati wa mchezo wa nusu fainali ya
kwanza kuwania Kombe la Mapinduzi utakaopigwa usiku katika uwanja wa Amaan.

Sterwart anayeinoa Azam FC na Sircovic mwalimu wa kikosi cha Simba, wote wanautazama mchezo wa leo kama indiketa ya kuelekea kutwaa ubingwa wa ligi kuu Tanzania Bara.


Timu hizo zimetinga hatua ya nusu fainali kwa mazingira tafauti, ambapo Azam iliongoza kundi B kwa kushinda michezo miwili na kutoka sare mmoja, huku Simba ikishinda miwili baada ya kuanza kwa kipigo
mikononi mwa Jamhuri ya Pemba.

Hata hivyo, wakati mashabiki na wadau wa soka kisiwani hapa wakiikejeli Simba kwamba imeingia hatua hiyo kwa mbeleko, kocha wa timu hiyo Sircovic hataki kuamini maneno hayo, akijigamba kuwa
wachezaji wake walijituma katika mchezo wa mwisho dhidi ya Miembeni United, hivyo walistahili kushinda.

"Ninavyofahamu ni kwamba Simba imeshinda, sijui kama kulikuwa na mpango uliofanywa ili iachiwe bao, lakini kwa namna lilivyofungwa, siamini kuwepo kitu kama hicho, kila mtu aliwaona vijana wangu waking'ara", alijitetea Mserbia huyo kwa Kingereza cha taabu.

Katika pambano hilo dhidi ya Miembeni United, Simba ilivuka kwa bao la bahati nusu dakika kabla mchezo kumalizika, na kuibuka na ushindi wa mabao 4-3, na kocha huyo ameeleza matumaini yake ya kushinda leo licha ya kukiri ugumu wa timu wanayopambana nayo.

Naye Sterwart Hall, ambaye kikosi chake kiliisambaratisha Yanga iliyokuwa imeongezewa nguvu na wanandinga wake iliyowaacha Dar es Salaam, amesema hana wasiwasi na mchezo huo, ingawa hataidharau Simba.

"Nakiamini kikosi changu, siogopi timu katika mashindano haya, lakini pia sidharau, kwani kila mechi inakuwa na mazingira yake lakini kama mpiganaji, lengo langu ni kushinda", alihitimisha Muingereza huyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.