Habari za Punde

Zambia Yairusha Roho Kenya Netiboli

Na Kauthar Abdalla

 KATIKA kinyang'anyiro cha kuwania Kombe la Mapinduzi kwa mchezo wa netiboli, jana timu ya Nyayo Stars kutoka Kenya iliramba mchanga kwa kuchapwa mabao 47-44 na Zambia kwa upande wa wachezaji wanawake.

Katika michuano hiyo inayofanyika kwenye uwanja wa Gymkhana ikishirikisha timu za Afrika Mashariki na Kati, kina mama hao walionesha mchezo mzuri wakishambuliana kwa hamasa na kuwapa watazamaji burudani nzuri.


Ingawa hakukuwa na timu ya wenyeji Tanzania, mashabiki waliojazana uwanjani walijikuta wakigawana huku kila mmoja akijichagulia timu ya kushangiria kwa jinsi mabanati hao walivyodhihirisha vipaji vyao.

Wachezaji walioifungia Zambia mabao yake, ni Delilah Hamunyemba aliyemimina magoli 20, na Beauty Nakazwe ambae alipachika mabao 27.

Kwa upande wa Kenya, mchezaji Caroline Makhoha alifunga mabao 29, huku mwenzake Brigdit Nazala akimudu kumimina mabao 15.

Michuano hiyo inatarajiwa kutimua vumbi tena leo wakati Tanzania wanawake itakaporushana roho na Zambia wakati wa saa 9:30, kabla kina dada wa Uganda na Kenya kuendeshana mchakamchaka mnamo saa 10:45.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.