Balozi Seif asema urasimu utekelezaji makubaliano tatizo
Dk.Bilal atoa miezi minne kuweka sawa mambo
Na Mwandishi Wetu
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema mapendekezo ya Baraza la Mapinduzi ambayo yameungwa mkono na azimio la Baraza la Wawakilishi kulitoa suala la mafuta na gesi asilia katika orodha ya mambo ya Muungano tayari limewasilishwa serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya kuchukuliwa hatua.
Hayo yamesemwa na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, wakati wa kikao cha Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar huko jijini Dar es Salaam, chini ya Mwenyekiti wake Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal.
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zimeeleza kwamba suala hilo pia lilijadiliwa wakati wa kikao hicho, kilichowahusisha Mawaziri, Makatibu Wakuu, Watendaji wa Serikali wa pande hizo, wakiwemo pia Wataalamu kwenye ukumbi wa Blue Pearl Ubungo Plaza jijini Dar es salaam.
Hata hivyo, baada ya kumalizika kikao hicho, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (anayeshughulikia Muungano), Samia Suluhu Hassan alisema suala la mafuta na gesi asilia katika kikao hicho lilijadiliwa lakini halikuweza kufikiwa muafaka.
Waziri Samia alisema kwamba baada ya kikao hicho kushindwa kufikia maamuzi juu ya suala hilo, sasa litafikishwa kwa viongozi wa juu serikalini, ili kupatiwa ufumbuzi.
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Baraza la Mapinduzi ilitoa pendekezo ambalo liliungwa mkono kwa asilimia 100 na Baraza la Wawakilishi, ilipendekeza suala la mafuta na gesi asilia litolewe katika orodha ya mambo ya Muungano, ili maliasili hiyo iweze kuwanufaisha Wazanzibari.
Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri Samia alisema mbali na suala hilo la mafuta na gesi asilia kikao hicho pia kilijadili kero mbali mbali za Muungano, ikiwemo suala la Ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Uvuvi katika Ukanda wa Bahari Kuu na Ushirikiano wa Zanzibar na Taasisi za Nje.
Mambao mengine yaliyozungumziwa alisema, ni ajira kwa Watumishi wa Zanzibar katika Taasisi za Muungano, Mgawanyo wa Mapato yatokanayo na faida ya Benki Kuu na Malalamiko ya Wafanyabiashara kutozwa kodi mara mbili pale bidhaa zao wanapoziingiza Tanzania Bara.
Mengina ni Usajili wa vyombo vya moto, ongezeko la gharama za umeme kutoka Tanesco kwendaShirika la Umeme Zanzibar (ZECO) pamoja na vitendo vya uharamia katika bahari ya Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya kikao hicho, Mwenyekiti wa Kikao hicho, Dk. Mohammed Gharib Bilal aliagiza mamlaka zinazohusika kutoa maelekezo katika kipindi cha miezi minne kuhusu suala la utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia.
Nae, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi alisisitiza haja ya kuwa na ratiba maalum ya vikao pamoja na kupunguza urasimu wa utekelezaji wa maamuzi yanayofikiwa katika vikao hivyo vya pamoja.
Balozi Seif alisema hatua hiyo itapunguza kero zilizopo na hatimaye kuamsha ari ya kuimarisha Muungano kwa maslahi ya pande zote mbili za Muungano huo.
“Nirahisishieni kazi ndani ya Baraza la Wawakilishi kwani wajumbe wake wako kitu kimoja, na hakuna mjumbe wa CCM wala CUF katika suala lolote linalohusu Muuungano ”, alikaririwa Balozi Seif ndani ya kikao hicho.
Mapema Wajumbe wa kikao hicho walikubaliana kuthibitisha kumbu kumbu za Kikao cha Kamati ya pamoja ya SMT na SMZ cha tarehe 2 Juni mwaka 2010, kilichokutana hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar.
Halikadhalika Wajumbe hao walipitia taarifa ya Utekelezaji wa yatokanayo na kikao hicho ambayo ni ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi asilia, Uvuvi katika ukanda wa Bahari Kuu na Ushirikiano wa Zanzibar na Taasisi za Nje.
Taarifa nyengine ni ajira kwa Watumishi wa Zanzibar katika taasisi za Muungano, mgawanyo wa Mapato yatokanayo na faida ya Benki Kuu (BOT), Malalamiko ya Wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili waingizapo bidhaa zao Tanzania Bara, usajili wa vyombo vya moto, likiwemo pia ongezeko la gharama za umeme kutoka TANESCO kwenda Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO) na Uharamiawa na utekaji nyara meli.
Katika kikao hicho, upande wa Wajumbe wa Serikali ya Muungano uliongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Kayanza Peter Pinda, wakati ule wa Zanzibar uliongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.
No comments:
Post a Comment