Habari za Punde

Miche ya Mikarafuu 34,000 Yapandwa Pemba

Na Bakar Mussa, Pemba

JUMLA ya miche ya mikarafuu 34,000 imepandwa katika maeneo mbali mbali kisiwani Pemba, katika msimu wa mvua za Masika zilizopita na miche 160,000 sawa na asilimia 54 ya lengo imeshazalishwa na inatarajiwa kutolewa katika msimu ujao.

Hayo yalielezwa na Ofisa Mdhamini Wizara ya Kilimo na Maliasili Pemba, Dk. Suleiman Shehe Mohammed, alipozungumza na mwandishi wa habari hizi juu ya hatua mbali mbali wanazochukua katika Wizara yake juu ya kuliimarisha zao la karafuu.


Alisema katika kufikia lengo kamili la kuzalisha miche ya mikarafuu 300,000 tayari Idara yake imeshakusanya matende na kuyaatika katika vitalu vyake mbali mbali kisiwani Pemba, ingawaje miche hiyo haitaweza kutolewa msimu ujao wa mvua za Masika kutokana na kutofikia kiwango cha kupandwa.

Alifahamisha kuwa pamoja na hilo matayarisho ya upandaji wa miche ya mikarafuu msimu ujao tayari yameshaanza kwa kuwaelimisha mabwana Shamba wa Wilaya zote za Pemba, kuanza kukusanya taarifa kwa kukagua maeneo ya kila mkulima anayehitaji miche kwa kumpimia eneo lake kwa ajili ya kupata mahitaji halisi ya miche inayohitajika kwa kila eneo.

Dk. Suleiman alisema pamoja na mafunzo hayo pia walitakiwa mabwana shamba, kuwaelekeza wakulima utaratibu mzuri wa mashimo yanayotakiwa kwa ajili ya kupanda mikarafuu ikiwa ni pamoja na kuanza kuwapimia maeneo ya upandaji baina ya mche na mche.

Alieleza kuwa katika kuhifadhi mikarafuu na kuhakikisha bado inabaki salama kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla , Wizara imechukuwa hatua za kupunguza ukataji wa mikarafuu kwa kufanya doria kila eneo pamoja na kutoa matangazo ya kuwataka wananchi kuacha tabia ya kukata mikarafuu mibichi, na ile iliyokwisha kauka lazima kuwepo na kibali kutoka mamlaka husika.

Hivyo, aliwataka wananchi na wakulima wa mikarafuu , kuwa walinzi wakubwa kwa wale ambao wanahusika na shughuli za uhujumu wa miti hiyo, iwe kwa kukata miti ama kuni , kwani bado Mikarafuu ni hazina ya Wazanzibari.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.