Habari za Punde

Tendwa Afadhaishwa na ‘Timua timua’ kwa Wanasiasa

Na Margreth Kinabo, Maelezo

MSAJILI wa Vyama Vya Siasa, John Tendwa amesema ofisi yake inafikiria kuweza kubadilisha mifumo ya uchaguzi kwa kufikiria nafasi na haki za msingi za mpigakura dhidi ya chama kinapomfukuza uanachama mbunge.

Kauli hiyo aliitoa jana jana wakati akizungumza na waandishi wa habari Ikulu jijini Dares Salaam mara baada ya kuapishwa kwa viongozi wapya wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC), ambapo alisema suala la kufukuzwa uanachama mbunge si geni lilishatokea hata katika mfumo wa chama kimoja.


Tendwa alitoa kauli hiyo mara baada ya kuulizwa suali na waandishi wa habari kuhusiana na kitendo cha Mbunge wa Jimbo la Wawi, Hamad Rashid Mohammed kufukuzwa uanachama na Baraza Kuu la Uongozi la Chama cha Wananchi (CUF) hali ilimfanya kupoteza nafasi ya Ubunge wake.

Alisema umefika wakati katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi inapotokea hali ya namna hiyo, lazima mpiga kura afikiriwe na chama juu ya sifa na haki za msingi dhidi ya chama.

“Tunafikiria tuweze kubadilisha mifumo hiyo ya uchaguzi kwa kuangalia mbunge na lazima tumfikirie mpigakura. lazima tuangalie hali ya uchumi”, alisema Tendwa.

Alisema kitendo hicho kinasababisha gharama kwa serikali na wadau wengine mfano taasisi yake ambayo haikutarajiwa hata katika bajeti.

Tendwa aliongeza kuwa inapotakiwa kufanyika uchaguzi mwingine zinahitajika fedha nyingi ambapo wakati fulani alisema zinaweza kufikia shilingi bilioni 19, hata hivyo hazitoshi.

Aidha alisema kuwa kifedha bado kitendo hicho kililiweka taifa katika mshtuko mkubwa kwa kuwa gharama ya kufanyika kwa uchaguzi mwingine ni kubwa.

Alihoji kuwa maamuzi hayo yanapofanyika hawakuona fursa ya mpigakura ana haki gani ya kumtambua mbunge wake? je chama kinafaidika nini? Alisema wataangalia kama taratibu zilifuatwa na chama ili waweze kushauri

Tendwa alisema suala hilo limekuwa ni tabia na desturi, hivyo ni jambo linapaswa kuangalia mbele ni hatua gani zinapaswa kuchukuliwa kwa kuwa kitendo hicho si kujenga demokrasia bali ni kuwafanya wanachama kuwa na utii wa uwoga ndani ya chama.

Naye Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo akizungumzuia suala hilo alisema kitendo hicho cha kumwondoa mbunge katikati ya muda kinaleta matatizo makubwa ndani ya vyama, hivyo alivishauri vyama kuheshimu sheria na taratibu za mtu kumaliza muda wake.

Hivi karibuni Chama cha NCCR – MAGEUZI nacho kilimvua uanachama, Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini, David Kafulila kwa madai ya utomvu wa nidhamu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.