Habari za Punde

CCM Yamnadi Raza Uzini

Na Mwantanga Ame

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Amani Abeid Karume amesema mgombea wa chama hicho kwenye uchaguzi mdogo jimbo la Uzini, Mohammed Raza, ana kila sababu ya kushinda kwani kura za maoni zimebainisha ushidi wa kishindo.

Dk. Karume aliyasema hayo jana kwenye uzinduzi kampeni kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa jimbo la Uzini wilaya ya Kati Unguja, zilizofanyika katika kiwanja cha skuli ya Uzini.


Dk. Karume alisema kura za maoni wakati wa kumtafuta mgombea wanachama wengi wa jimbo hilo wameonesha wazi kuwa CCM itaibuka na ushindi wa kishindo, hivyo ni vyema wananchi wakahakikisha wanaweka historia kwa kukipa ushindi mnono chama hicho.

Alisema CCM kumteua mgombea huyo, ilizingatia misingi ya demokrasia kwa kuhakikisha inalirejesha jina la Raza kwa kutambua kuwa ndio chaguo la wanachama wa jimbo hilo.

Alisema CCM inazingatia na kutambua haki za wanachama sio kama vilivyo vyama vyengine vinavyoamua kutengua majina ya wagombea hata kama wanachama waliwapa ridhaa ya kutoka kwa wananchi.

Makamu huyo aliwataka wananchi na wanachama wa CCM, Uzini wasifanye kosa kwa kuchagua mgombea wa chama kingine bali kura zote wamiminie Raza ambaye ni mkereketwa na mtu atakayeleta maendeleo.

Dk. Karume alieleza kuwa CCM ndio chama pekee kilichosimamia amani, umoja na utulivu wa nchi na ndio maana hivi sasa Zanzibar ipo katika amani ya hali ya juu kiasi cha inaifanya nchi kuendelea.

Akijitambulisha kwa wananchi kwenye mkutano huo, Raza alisema endapo atapewa ridhaa atahakikisha anaitekeleza vyema ilani ya CCM, kwani hakuna linaloshindikana ndani ya chama hicho.

“Msibahatishe wanachama wa CCM kuwapa upinzani, tambueni kuwa CCM Jimbo la Uzini ni Raza kwani CCM uwezo inao nia ipo na sioni sababu kwa nini msinipe kura hizo kelele za wapinzani ni sawa na za mlango hazimkeri mwenye nyumba iambieni dunia Uzini ni CCM”, Raza alisema.

Kwa upande wake katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama alisema chama hicho hakina Mwari katika uchaguzi, bali inaingia katika kinyang’anyiro hicho ikiwa na mchumba ambae hataruhusu kuingia mpita njia kushika jimbo la Uzini.

Nae Makamu wa CCM Tanzania Bara, Pius Msekwa akitoa salamu zake alisema, wanachama wa CCM wanalazimika kukumbuka ahadi yao kwa kuona wanakuwa waaminifu kwa kuhakikisha wakati wa ushindani wanapiga kura kwa Chama chao kwa kumchagua Raza.

Alisema haiwezekani mrithi wa CCM akatoka upinzani na ni vyema kutumia nafasi yao hiyo kuona wanamchagua mgombea huyo kwa kukumbuka kuwa Chama kinatarajia kufanya uchaguzi wa ndani ya Chama ikiwa ni hatua ya kupata viongozi bora.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai akitoa salamu zake alisema upizani licha ya kuanza mwanzo kampeni lakini CCM itahakikisha inawapita njiani kwa vile hawana waliwezalo na Jimbo hilo litabakia kuwa ngome ya CCM.

1 comment:

  1. Hivi huyu jamaa ana elimu gani? au ndio yale yale
    Ni mwenzetu,..hana majungu, mpenda watu, mzoefu..

    Kumbukeni, mshkaji alishawahi kuhudumu kama mshauri wa rais wa mambo ya michezo wakati wa ushabik(1995-2000).. asije akatuletea tena design zile pale!!!

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.