Habari za Punde

Wajasiriamali Waelimishwa Kutengeneza Bidhaa Bora

Na Othman Maulid

JUMUIA ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima Zanzibar, inaendelea kutoa mafunzo ya awamu ya pili kwa wajasiriamali kupitia mpango wa uendelezaji mitaji wa ‘Faidika kibiashara’ BDG.

Mafunzo hayo yanayotolewa ukumbi wa Kituo cha Elimu Mbadala Rahaleo Mjini Zanzibar, pia yanawaelimisha wajasiriamali hao namna ya kuzalisha bidhaa bora pamoja na ufungaji mzuri wa bidhaa zao unaokubalika katika viwango vya kitaifa na kimataifa.


Chama hicho kimeeleza kuwa mafunzo hayo ni kwa ajili ya wajasiriamali wa Mkoa wa Mjini Magharibi, ambapo taaluma kama hiyo inatolewa kwa wajasiriamali wa Mikoa ya Kusini na Kaskazini Unguja.

Akifungua mafunzo hayo, Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Zanzibar, Ali Aboud Mzee, ametoa wito kwa wafanyabiashara na wajasiriamali kujiunga na Jumuiya hiyo ili waweze kutumia fursa nzuri za kibiashara zizopo nchini na nje ya nchi.

Mkufunzi wa mafunzo hayo ameeleza kuwa pamoja na mambo mengine, wajasiriamali hao watasaidiwa mafunzo ya kutafuta masoko, pamoja na kutayarisha vyema bidhaa zao ili ziweze kufikia viwango vya kitaifa na kimataifa.

Baadhi ya wajasiriamali imegundulika kuwa bidhaa zao zinakosa masoko kwa kutotambulika, jambo ambalo limeelezwa kusababishwa na kuwa chini kiviwango na ukosefu wa elimu ya kufunga bidhaa ‘packaging’ na masoko kwa wajasiriamali.

Afisa Fedha wa Jumuiya hiyo, Husna Ahmed Mohamed, alisema kuwa tatizo la wafanyabiashara wa Zanzibar sio ukosefu wa soko, bali ni ubora wa bidhaa wanazozalisha, jambo ambalo limewekewa mikakati na Jumuiya hiyo ili kuwaendeleza wafanyabiashara waweze kuzalisha bidhaa zitakazojiuza katika masoko ya ndani na nje ya nje.

Wajasiriamali 69 wameshiriki mafunzo hayo wakiwemo wanaozalisha bidhaa za ukili, wafuma mazulia, wasokota kamba, watengeneza sabuni na bidhaa nyengine za viungo.

Mafunzo hayo yanafanyika chini ya msaada wa Benki ya watu wa Zanzibar Ltd (PBZ) na Benki ya NMB.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.