OFISI ya Makamu wa Pili wa Rais imetoa pongezi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein kutokana na utaratibu aliouanzisha wa kukutana na Mawizara na kujadili mpango Kazi wa mawizara wa mwaka na utekelezaji wake kwa kila robo mwaka.
Uongozi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais chini ya Waziri wake, Mohammed Aboud, ulieleza hayo ulipokutana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu mjini Zanzibar ambapo pia, Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd alihudhuria kikao hicho.
Mkutano huo ni muendelezo wa kukutana na Wizara za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuangalia Mpango Kazi wa utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2011/2012 kwa kipindi cha robo ya kwanza na ya pili ya mwaka.
Akitoa utangulizi juu ya taarifa ya utekelezaji wa Bajeti ya Ofisi hiyo, waziri Mohamed Aboud alisema Ofisi hiyo imejiwekea dira yake ambayo ni kuwa na serikali yenye kutoa huduma bora kwa jamii na yenye uhimili mzuri wa uchumi.
Pamoja na umoja na kusimamia utekelezaji wa shughuli za serikali katika sekta zote za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar mambo ya Muungano kwa kufuata maagizo ya Katiba, sheria na taratibu pamoja na kuhakikisha kufuata misingi ya haki za binadamu na ushirikishwaji.
Waziri huyo alieleza kuwa dira na dhamira hiyo ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais inaenda sambamba na dira ya Maendeleo 2020, Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUZA II), na Maendeleo ya Milenia (MDGs).
Aidha, ofisi imeratibu masuala mbali mbali yanayohusu changamoto za Muungano kupitia vikao vya mashirikiano vya kisekta kwa lengo la kufanya mahusiano katika utendaji kazi na kudumisha Muungano.
Ofisi kwa kushirikiana na Mawizara na taasisi mbali mbali za serikali imefanikiwa kukusanya na kuandaa ripoti ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM mwaka 2010/2015.
Waziri huyo alieleza kuwa Ofisi imeratibu kwa mafanikio makubwa masuala ya utafiti, ikiwa ni pamoja na kuziunganisha COSTECH na watafiti wa ndani pamoja na Taasisi mbali mbali zinazojihusisha na mambo ya utafiti nchini.
Aidha, hatua za kukihamisha kiwanda cha Mpiga Chapa Mkuu wa serikali kutoka eneo la Saateni kwenda Maruhubi ambapo Ofisi inakusudia kuanza matengenezo ya majengo ya kilichokuwa kiwanda cha Sigara, Maruhubi.
Pamoja na hayo, Ofisi hiyo ilieleza kuwa imepokea na kuratibu kwa makini misaada yote iliyotolewa na taasisi mbali mbali za ndani na nje ya nchi na kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya kukabiliana na maafa kwa kupitia njia mbali mbali ikiwemo vyombo vya habari.
Pia, Waziri huo alieleza hatua zilizochukuliwa na Ofisi hiyo katika kuratibu kazi za Baraza la Wawakilishi ikiwemo kupitisha miswada ya sheria, kufuatialia utendaji wa kazi za taasisi za SMZ, Kamati za Kiuchumi, kupitisha Bajeti ya Serikali na kuendeleza mashirikiano na Mabunge mengine duniani.
Nae Dk. Shein alitoa pongezi kwa Ofisi hiyo kwa kufanya kazi hiyo vizuri iliyopelekea kuwa na mjadala mzuri katika kuendeleza mipango na shughuli za ofisi hiyo.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alisisitiza mashirikiano katika utendaji wa kazi na kueleza kuwa kazi hiyo ni ya watu wote, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kutoa ushirikiano katika kufanikisha mustakbali mzuri wa maendeleo ya ofisi hiyo.
Wakati huo huo, Dk. Shein alikutana na Uongozi wa Wizara ya Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Wanawake na Watoto chini ya waziri wake Zainab Omar ambaye alieleza kuwa mikutano hiyo inasaidia kuibua changamoto za kiutendaji na kuzitafutia ufumbuzi katika wakati muwafaka.
Waziri huyo aliunga mkono hatua zinazochukuliwa na serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika utekelezaji wa ripoti ya Tume ya Mv. Spice Islander ya kuwawajibisha na kuwachukulia hatua za kisheria na kinidhamu wale wote waliotajwa katika kuhusiana na kadhia hiyo kubwa.
Uongozi huo ulizipongeza hatua za Dk. Shein za kufanya marekebisho ya mishahara na maposho kwa wafanyakazi na watumishi wote wa serikali kuanzia mwezi wa Oktoba 2011.
Wizara hiyo pia, ilieleza mambo muhimu iliyoyatekeleza ambayo yalipewa kipaumbele zaidi kwa ajili ya kuharakisha maendeleo na kuwahudumia Wazee, Wanawake, Vijana, Watoto na Ustawi wa Jamii kwa jumla.
Kwa upande wa wazee wizara hiyo ilieleza kuwa imeweza kuwaenzi na kuwahudumia ipasavyo wazee katika makaazi yao ikiwa ni pamoja na kuwaongezea maposho yao.
Kwa upande wa wanawake wizara imefanya uhamasishaji wa vikundi vya wanawake wajasiriamali kwa lengo la kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa kuanzisha SACCOS kwa kila wilaya ili ziwe msingi wa uanzishwaji wa Benki ya wanawake Zanzibar.
Nae Dk. Shein kwa upande wake alitoa pongezi kwa uongozi wa Wizara hiyo pamoja na watendaji wake wote kwa juhudi kubwa inazochukua katika kuendeleza na kuimarisha malengo na madhumuni ya Wizara hiyo.
Dk. Shein pia aliueleza uongozi huo kuwa ni matumaini yake makubwa kuwa vikao hivyo vitakuwa ni chachu katika utendaji wao wa kazi kwa ufanisi zaidi na uelewa wa mambo yanayohusiana na wizara hiyo.


No comments:
Post a Comment