Habari za Punde

Habari Fupi za Siku Mbili za Mwanzo za Tamasha la Sauti za Busara


Tamasha la Sauti za Busara mwaka huu liling’oa nanga tarehe tisa mwezi wa Februari kwa staili ya aina yake kwa ngoma za asili kama mdundiko, ngongoti, dufu na shangwe katika maandamano maarufu kama Carnival Parade ambayo yalianzia Kisonge Park saa kumi kamili jioni na kuishia Ngome Kongwe saa kumi na mbili jioni.

Vitongoji mbalimbali Unguja vilipata bahati ya kujionea maandamano hayo kwani msafara huo ulikatiza katika vitongoji vya michenzani, Kisiwandui, Mkunazini, Mnazi Mmoja, Vuga na Shanghani kabla ya kutia nanga Ngome Kongwe.


Baada ya hapo, siku nne za burudani na muziki mfululizo katika visiwa vya Unguja zilianza rasmi. Vikundi kadhaa vimetoa burudani ndani ya viwanja vya Ngome Kongwe, ambavyo ni Mkota Spirit Dancers kutoka Pemba, Swahili Vibes, Shirikisho Sanaa, Tandaa Traditional Group, Wanafunzi wa SOS, Ary Morais (Cape Verde/Norway) na Mashauzi Classic modern taarab ya Tanzania ikiongozwa na Isha Mashauzi.

Kikundi kutoka Pemba, Mkota Spirit Dancers kilifanya shoo ya aina yake iliyopambwa na uvaaji wa kiasili na nyimbo zao za Kiswahili cha aina yakipekee kama ‘Uganga Ukuu’, ‘Ng’ombe alia Baa’, ‘Ukaruka Mgongowa’ na ‘Bamba la Mvumo’.
Jike la Simba, Isha Mashauzi aliwarusha wakazi na wageni kwa uimbaji wake na uchezaji wa nyimbo zake maarufu kama ‘Mama Nipe Radhi’ na ‘Tugawane Ustaarabu’ ambazo ziliwafanya hata wasioelewa alichokuwa akiimba kuvuja jasho kutokana na kucheza mwanzo mwisho.

Pamoja na muziki kutoka katika vikundi mbalimbali, katika viunga vya Ngome Kongwe, vinaonyeshwa vipande vya video za aina mbalimbali ya muziki kama vile Taarab, Kuduro, Hip Hop, Bongo Flava, Mchiriku na hili litakuwa likifanyika kila siku.
Siku ya pili, mwanamuziki Hanitra kutoka Madagascar alifungua show na kufuatwa na Tausi Women Taarab pamoja na Bi Kidude aliyekonga mioyo mashabiki wake. Kikundi kutoka Sudan, Camirata Group kilifuata na baadaye Ogoya Nengo alipanda jukwaani. Mkongwe huyo aliwashangaza wengi kwa staili yake ya kucheza huku akionekana kuwa na pumzi ya kutosha.

Naye Waziri wa utalii wa Kenya Mheshimiwa Najib Balala pia alipata wakati wa kuzungumza katika tamasha na kuelezea zaidi kuhusu mpango wa ushirikiano baina ya Lamu Festival ya Kenya na Sauti za Busara. Alimkabidhi mkurugenzi wa tamasha bwana Yusuf Mahmoud kitabu maalum kuhusu Lamu.

Utamaduni JKU kutoka Zanzibar na Kozman Ti Dalon kutoka kisiwa cha Reunion walifuata baadaye. Fredy Massamba kutoka Congo aliwatumbuiza mashabiki wa tamasaha na wimbo wake maarufu ‘Lobelanga’. Aliwahamasisha kuhusu kudumisha amani na upendo.Super Mazembe kutoka Kenya walifunga show ya siku ya pili ya tamasaha kwa shangwe na vigelegele kwani nyimbo zao zimejulikana kanda la Afrika.Wanamuziki walicheza dansi staili ya lingala na waliimba nyimbo kama ‘Kasongo’ na ‘Shauri Yako’ zilizo waacha waliohudhuria kutaka show nyingine.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.