Habari za Punde

Mfumo wa Uombaji Uraia TZ Kubadilishwa

Na Kunze Mswanyama, Dodoma

WIZARA ya Mambo ya Ndani, ipo kwenye harakati za kuboresha mfumo wa uombaji uraia pamoja na vyeti vya uraia ili viwe kwenye mfumo wa kielekroniki hali itakayozidisha usalama.

Naibu waziri wa Mambo ya Ndani, Khamis Kagasheki, alieleza hayo jana Bungeni mjini Dodoma alipokuwa akijibu suali la Dk. Festus Limbu (Magu), aliyetaka kujua sababu za kuondolewa pasi kwa Watanzania wanaoingia Afrika Kusini, ambapo zaidi ya 100 wamerejeshwa kutokana na kufoji hati za ukaazi.

Kagasheki alisema mfumo wa kielektroniki utazifanya hati hizo kuwa zenye usalama zaidi na kuepuka kughushiwa pamoja na kuwa imara zaidi.


Katika suali lake hilo Dk. Limbu alisema zipo taarifa kuwa baadhi ya vijana hughushi vyeti vya uraia ili kupata viza hiyo, ambapo Naibu huyo alisema Idara Uhamiaji inaendesha ukaguzi maalumu ili kubaini uhalali wa tuhuma hizo.

Alifahamisha kuwa kwa mujibu wa sheria ya uhamiaji namba 6 ya mwaka 1995 na kanuni zake za mwaka 1997, serikali inatakiwa kuendesha misako ili kuwabaini wahamiaji haramu wote na kuwachukulia hatua kali.

Balozi Kagasheki aliwataka watanzania kufahamu kuwa tatizo hilo ni la dunia nzima na hivyo kila mwananchi anatakiwa awe mzalendo kwa kutoa taarifa kwa vyombo vya dola ili kuwakamata na kuwafikisha mahakamani ili mkondo wa sheria ufuate.

Alisisitiza kuwa mfumo wa usajili wa vitambulisho vya taifa ulioanza hivi karibuni na kuhusisha awamu ya kwanza kwa watumishi wa umma ambapo itasaida zaidi kuwafahamu wasiokuwa wananchi halali za Tanzania.

Wakati huo huo, Balozi Kagasheki amesikitishwa na taarifa za kuwepo na udhalilishaji mkubwa Magerezani na Vyuo vya Mafunzo ambapo aliwataka askari wote kutowadhalilisha wafungwa na mahabusu kwa kuwa bado wana haki za binadamu.

Katika suali lililoulizwa na Mhonga Luhanywa (Viti Maalum) aliyetaka kujua kuwa matendo ya ukatili na ukiukwaji wa haki za binadamu zinazovunjwa na baadhi ya askari Magereza ambapo huvuliwa nguo zote na kisha kurukishwa kichura ikiwa ni vitendo vya ukaguzi ambapo misingi ya haki za binadamu haziruhusu.

Katika swali hilo Luhanywa alitoa mfano wa gereza la Bangwe mkoani Kigoma ambapo wanawake wanaoingia huvuliwa nguo zote hali ambayo ni udhalilishaji.

“Ndio mara ya kwanza kusikia taarifa hizo za kushtua kuhusu gereza hilo. tumefuatilia bila kupata ushahidi huo, namuomba Mbunge kama anao ushahidi wa jambo hilo anipatie mara moja, bila kuwabaini askari hao ni vigumu kuwaadhibu kama aelezavyo Mbunge”,alisema Balozi Kagasheki.

Alisema wahalifu wanapoingia na wawapo gerezani zipo kanuni zinazolinda na kuthamini haki za utu wao chini ya kanuni za kudumu za uendeshaji Jeshi la Magereza za mwaka 1986 ambazo hazimruhusu askari kudharau au kutothamini na kumdhalilisha au kumtesa mfungwa, hatua kali za kisheria huchukuliwa mara moja dhidi ya askari atakayebainika kuwa amekiuka sheria hizo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.