Habari za Punde

Mtendaji Kizimbani kwa Rushwa

Na Jumbe Ismailly, Singida

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida imepandisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, ofisa mtendaji wa kijiji cha Misake, kata ya Minyughe, wilayani hapa, Omari Bakari Mandi (49) kwa tuhuma ya kuomba na kupokea rushwa ya jumla ya shilingi 115,000.

Mwendesha mashitaka, Mwanasheria wa TAKUKURU Mkoa wa Singida,Wilsoni Ntiro alidai kwamba Novemba 17,mwaka jana, majira yasiyofahamika mshitakiwa huyo alimwomba Mwenyekiti wa Kitongoji cha Makilawa, Joseph Ipunze Dwash rushwa ya shilingi 40,000/=ili aweze kumbakisha kwenye nafasi yake.


Kwa mujibu wa mwanasheria huyo akiwa mtumishi wa umma, Mandi alitenda kosa hilo huku akijua wazi kwamba ni kinyume na kifungu cha sheria ya makosa ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11/2007.

Hata hivyo ofisa mtendaji huyo wa Kijiji licha ya kuomba kiasi hicho chja fedha, lakini aliambulia kuomba tu, na hakufanikiwa kupokea kiasi hicho cha fedha alichokuwa akikiomba.

Aidha mshitakiwa Mandi hata hivyo alikana shitaka hilo na yupo mahabusu baada ya kukosa watu wa kumdhamini hadi Februari 14, mwaka huu kesi hiyo itakaposikilizwa hoja za awali.

Katika shitaka la pili, Mwendesha mashitaka wa TAKUKURU alidai mbele ya hakimu wa Mahakama hiyo, Ruth Massamu kuwa Disemba 10 mwaka jana majira yasiyofahamika mshitakiwa alimwomba tena mwenyekiti wa kitongoji cha Makilawa Dwash rushwa ya shilingi 75,000 ili asimwondoe kwenye nafasi yake hiyo.

Hata hivyo ofisa huyo wa serikali ya kijiji hakuweza kupokea kiasi hicho cha rushwa kutokana na kuzungushwa na mtu aliyemwomba kufanya hivyo.

Hata hivyo mshitakiwa huyo alikana pia shitaka hilo na yupo mahabusu baada ya kukosa wadhamini hadi Februari 14, mwaka huu kesi hiyo itakaposomewa hoja za awali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.