Habari za Punde

Ali Mbarouk Mshimba - Mgombea Uwakilishi Uzini

MWISHONI mwa wiki Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilizindua kampeni zake za uchuguzi katika Jimbo la Uzini ikiwa ni maandalizi ya kumpata mwakilishi katika jimbo hilo.

Uchaguzi huo unakuja ikiwa ni baada yakiti hicho kuwa wazi kutokana na aliyekuwa mbunge wa Jimbo hilo, Musa Khamis Silima (CCM), kufariki dunia kutokana majeraha aliyoyapata kwenye ajali iliyotokea Agosti mwaka jana.

Tanzania Daima Jumapili, imeafanya mahojiano na mgombea uwakilishi kupitia CHADEMA, Ali Mbarouk Mshimba, ili kujua historia yake ikiwamo alipotokea kisiasa, changamoto mbalimbali ambazo anaona zinalikabili jimbo hilo na nini matarajio yake endapo atafanikiwa kuchaguliwa kuwa mbunge katika kuliendeleza jimbo hilo.


Mshimba anasema amezaliwa kijijini Uzini Aprili 10, mwaka 1966 na kusoma katika Shule ya Msingi Uzini darasa la kwanza na kumaliza la saba mwaka 1983, baadaye alijiunga na Shule ya Sekondari ya Fidel Castro iliyopo visiwani Pemba ambayo ina mchepuo wa kilimo.

Baada ya hapo alijiunga na Jeshi la Kujenga Uchumi mwaka 1988 hadi 1989 na alipotoka hapo akapata kazi ya ualimu mwaka 1990 katika Shule ya Sekondai Mchangani ambayo ndio anaendelea nayo hadi leo ambapo amechukua likizo ya miezi mitatu bila malipo kwa ajili ya kufanya kampeni.

Kwenye siasa

Mshimba anasema ameanza kuingia kwenye siasa tangu mwaka 1990 ambapo alikuwa Katibu wa vijana Tawi la Uzini na wakati huohuo alikuwa akikaimu nafasi hiyo ya ukatibu katika Jimbo la Tunduni (CCM).

Ilipofika mwaka 1995 aligombea kiti cha uwakilishi Jimbo la Uzini kupitia CCM ambapo katika kura za maoni hakufanikiwa na badala yake alipitishwa Tafan Kassim Mzee.

Pamoja na kushindwa katika kinyang’anyiro hicho aliendelea na harakati zake za siasa ambapo kwa mara nyingine aligombea nafasi ya Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) akachuana na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Dk. Emmanuel Nchimbi ambapo hata hivyo hakufanikiwa kuipata nafasi hiyo iliyokwenda kwa mpinzani wake.

Anasema baada ya kushindwa kwenye uchaguzi huo aliendelea kuwa mjumbe kwenye kamati za mikakati na kutokana ukali wake dhidi ya wale waliokuwa wakienda kinyume na maadili ya chama alianza kuchukiwa na kupigwa vita.

Anaongeza kuwa alipoona mambo yanamwendea kombo kutokana na msimamo wake aliamua kujiondoa ndani ya chama hicho ambapo mwaka 2010 alijiunga na CHADEMA kilichompa fursa ya kuwania nafasi ya ubunge katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka huo.

Mgombea huyu anasema historia ya jimbo hilo kwa muda mrefu lipo mikononi mwa CCM hivyo hata alipoingia kwenye kinyang’anyiro cha ubunge mwaka 2010 hakuweza kufurukuta mbele ya mgombea wa chama hicho tawala.

Mshimba anasema CCM ilijikuta ikifanya ufisadi wa kidemokrasia katika jimbo hilo ambapo iliwajengea wananchi kwamba hakuna chama chochote zaidi kitakachoweza kuwaletea maendeleo zaidi ya CCM.

Hivyo katika kipindi hiki anasema harakati za kulichukua Jimbo hilo zinaendelea na kwamba tayari wananchi wameanza kuzinduka na kuona kwamba hata vyama vingine vinaweza kuwaletea maendeleo baada ya muda mrefu tangu kutokea mapinduzi jimbo hilo halijapiga hatua za maendeleo kama ilivyotarajiwa.

Mshimba anasema jimbo hilo ni la pili kutambuliwa katika vuguvugu la kuleta mapinduzi ya Zanzibar likitanguliwa na lile la Donge ambapo kwa matarajio ndio lingetakiwa kuongoza kimaendeleo kutokana na mchango ambao limeweza kuutoa katika kuwafanya Wazanzibari kuwa huru.

Anasema hapo ndipo iliamriwa Wazanzibari kupata huduma kama za afya na elimu bure lakini hivi sasa hali haipo hivyo na badala yake huduma hizo zimekuwa ni gharama kwao jambo ambalo wengine wameshindwa kabisa kuzimudu.

Ahadi zake

Anasema endapo atachaguliwa kuwa mbunge ataendeleza malengo ya uanzishwaji wa Chama cha Afro Shirazi ikiwemo kuwapatia wananchi makazi bora jambo ambalo hayati Aman Abeid Karume alianza kulitekeleza kwa kuwajengea wananchi waliokuwa na hali duni kimaisha nyumba za magorofa.

Mshimba anasema zoezi hilo la ujenzi wa nyumba za maghorofa Marehemu Karume amekufa nalo kwani hakuna aliyeliendeleza licha ya kuwa na manufaa makubwa kwa wakazi wa kisiwa hicho.

Anasema atapambana kuhakikisha gharama za vifaa vya ujenzi zinashushwa ikiwemo kuziondolea kodi ili wananchi wamudu kununua mabati, simenti na vifaa vinginevyo.

Anaongeza kuwa atalishughulikia suala la kutoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi chuo kikuu. anasema hivi sasa gharama za kuwasomesha wanafunzi zimepanda sana na matokeo yake watoto wengi wanaomaliza elimu ya msingi hukosa nafasi ya kuendelea mbele pamoja kukosa fursa ya kupata kazi.

Mshimba anasema atatetea katika Baraza la Uwakilishi mitaaala iliyopo ibadilishwe ili kumjengea mhitimu uwezo wa kujiajiri mwenyewe pindi amalizapo masomo yake badala ya kusubiri kuajiriwa kwenye sekta ya umma au binafsi.

Kuhusu sekta ya afya, anasema atashughulikia suala la upatikanaji wa madaktari katika jimbo hilo ambalo kwa sasa lina vituo vingi vya afya lakini halina madaktari zaidi wanahudumia na manesi na wauguzi.

Kutokana na hali hii anasema wagonjwa wamejikuta wakiandikiwa dawa bila kuchukuliwa vipimo jambo ambalo ni hatari kwa afya zao, kwani wanaweza wakajikuta wanatibiwa magonjwa ambayo si ynayowasumbua

Kutatua matatizo ya Uzini

Mshimba anasema tatizo kubwa kwa sasa lililopo Uzini ni la upatikanaji wa maji safi na salama, ambapo wakazi hao amekuwa wakitembea umbali mrefu kuyafuata na maji yenyewe ni ya kisima na kuongeza kwamba siku mbili kabla ya kuanza kampeni ndiyo yameanza kutoka.

Katika hilo anasema atahakikisha maji yanapatikana wakati wote na kwa yale ya visima atahakikisha yanawekwa katika hali ya usafi badala ya sasa hivi vipo wazi na hivyo kujikuta yakiingia uchafu na wakati mwingine kunywewa na wanyama kama ng’ombe, jambo ambalo ni hatari kwa afya zao.

Katika Kilimo ambacho amedai ndio shughuli kubwa ambayo inaweza kuwaletea maendeleo wananchi wa Uzini, anasema atahakikisha pembejeo zinapatikana kiurahisi na kuwapatia masoko kirahisi tofauti na sasa hivi mkulima analazimika kusafiri hadi Unguja mjini kupeleka mazao yake.

Anasema atatengeneza mfumo wa masoko wa namna ya kuuza mazao hayo jimboni humo ikiwemo kuwa na kituo cha kuyakusanya kabla ya kupelekwa katika masoko makubwa.

Chanzo : Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.