Na Rajab Mkasaba, Ikulu
OFISI ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi imezipongeza juhudi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein katika kuwaletea maendeleo wananchi wote wa Unguja na Pemba na kueleza kuendelea kumuunga mkono ili Zanzibar iendelee kupata mafanikio makubwa ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Uongozi wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi chini ya Waziri wake, Dk. Mwinyihaji Makame, ulieleza hayo jana ulipokutana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu mjini Zanzibar.
Mkutano huo ni muendelezo wa Dk.Shein kukutana na Wizara za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuangalia Mpango Kazi wa utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2011/2012 kwa kipindi cha robo ya kwanza na ya pili ya mwaka.
Uongozi wa Ofisi hiyo ulieleza kuwa juhudi anazozichukua Dk. Shein, katika uongozi wake ni za kupigiwa mfano katika kuwaletea maendeleo endelevu wananchi wote ikiwa ni pamoja na kuangalia maslahi ya wafanyakazi wote wa sekta ya umma, wakulima na wananchi wote kwa jumla.
Aidha, uongozi huo ulieleza kuwa wananchi wa Zanzibar wamekuwa na matumaini na matarajio makubwa ya maendeleo kutokana na juhudi za uongozi wa Dk. Shein huku uongozi huo ukieleza kufarajika kwao na muendelezo wa vikao hivyo ambavyo vimeweza kuleta faida kubwa kwa viongozi, watendaji na wafanyakazi wote wa Serikali na kuweza kufanya kazi kwa kujituma.
Akisoma utangulizi juu ya taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Ofisi hiyo, Waziri Mwinyihaji alisema mkazo zaidi umewekwa na ofisi hiyo katika utekelezaji wa shughuli ambazo zinalenga kuinua hali za wananchi kiuchumi na kupunguza kero zao za kijamii.
Aidha, alisema Ofisi imeweza kuratibu na kusimamia utekelezaji wa malengo ya MKUZA, Dira 2020 na malengo ya Milenia pamoja na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010-2015.
Waziri huyo pia, alieleza kuwa vipaumbele vimewekwa katika kuendeleza Umoja wa Kitaifa na mshikamano, kuimarisha uwezo, utoaji wa huduma ikiwemo usafishaji wa miji na uendeshaji wa Serikali za Mitaa, Mikoa na Wilaya.
Pamoja na hayo Waziri Mwinyihaji alieleza kuwa Ofisi hiyo imeweka kipaumbele katika kuimarisha na kuongeza uwezo wa Idara Maalum za SMZ, Kuimarisha huduma bora katika vyuo vya Mafunzo pamoja na kupunguza msongamano.
Aidha, alisema kipaumbele chengine ni kuimarisha mfungamano wa Kikanda ili Wazanzibari waweze kutumia fursa za kiuchumi zinazotokana na Jumuiya za Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika na Jumuiya nyengine za Kikanda.
Pamoja na hayo uongozi huo ulieleza kuwa kipaumbele chengine ni kuwashajiisha Wazanzibari wanaoishi nchi za nje katika kushirikiana na kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi pamoja na kutoa elimu ya kujikinga na Maambukizi ya Ukimwi na VVU.
Akieleza miradi ya maendeleo ambayo Ofisi hiyo inaendelea na utekelezaji ambayo miongoni mwao ni pamoja na ujenzi wa chuo kipya cha Mafunzo Hanyegwa Mchana, ujenzi wa Hospitali Mpya ya Kikosi cha KMKM, Ujenzi wa Makao Makuu ya Valantia, mradi wa shamba la mboga mboga Bambi na ujenzi wa Ofisi za Wakuu wa Mikoa ya Kaskazini Unguja na Kusini Unguja.
Nae Dk. Shein kwa upande wake alitoa pongezi kwa Wafanyakazi, viongozi na watedaji wote wa afisi hiyo kwa kushirikiana pamoja na kufanya kazi hiyo nzuri waliyoiwasilisha.
Dk. Shein alisema miongoni mwa mambo muhimu aliyowahakikishia wananchi wakati wa hotuba yake ya tarehe 9 Novemba huko katika Baraza la Wawakilishi ilikuwa ni pamoja na kuangalia maslahi ya ya wafanyakazi wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kuwasaidia wakulima kwa kuwapunguzia ruzuku za mbegu, mbolea, dawa za kuulia magugu, kuwaajiri Mabibi Shamba na Mabwana Shamba pamoja na kuwasaidia huduma nyengine za ugani kwa asilimia 50 hadi 75.
Aidha, alieleza kuwa hatua nyengine ni pamoja na kuliimarisha zao la karafuu ambalo hivi sasa limeweza kuleta tija kubwa kwa wakulima pamoja na kuimarisha sekta nyengine za maendeleo zikiwemo huduma za afya na nyenginezo.
Wakati huo huo, Dk. Shein alikutana na Uongozi wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ulio chini ya Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kupitia Waziri wake Dk. Mwinyihaji Makame ambaye akisoma utangulizi wa taarifa juu ya utekelezaji wa malengo ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa alieleza vipaumbele ilivyoviweka.
Akizitaja Taasisi zilizo chini ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ambazo ni Ofisi za Mikoa yote ya Zanzibar, Wilaya, Halmashauri, baraza la Manispaa, Dk. Mwinyihaji alieleza vipaumbele ilivyoweka pamoja na Mkakati wake wa MKUZA II, Dira ya 2020 na Utekelezaji wake wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010-2015.
Kwa upande wa Baraza la Manispaa, uongozi huo ulieleza mikakati yake iliyojiwekea katika uzoaji taka na uondoaji mifugo ndani ya eneo la Manispaa ya Zanzibar kwa mashirikiano ya vikosi vya SMZ.
Licha ya mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa shughuli za Ofisi hiyo Dk. Mwinyihaji alieleza kuwa zipo baadhi ya changamoto inazozikabili ikiwa ni pamoja na uelewa mdogo wa wananchi juu ya kuuweka mji katika hali ya usafi, uvamizi wa ardhi, mizozo ya kupewa vibali bila ya kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa, elimu juu ya ulipaji kodi na changamoto nyenginezo.
Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee ambaye amekuwa akishiriki kikamilifu katika vikao hivyo tokea kuanza kwake alieleza haja ya kuendelea kufanyakazi kwa kushirikiana na kuwataka wafanyakazi wa Ofisi hiyo kuwa kioo kwa jamii.
Akizungumza na uongozi huo Dk. Shein alitoa pongezi kwa juhudi za uongozi huo kwa utendaji wao wa kazi na kueleza haja ya kuiimarisha miji ili iweze kuvutia ikiwemo manispaa ya mji wa Zanzibar pamoja na kuendelea kuzitafutia ufumbuzi kwa mashirikiano ya pamoja changamoto mbali mbali zilizopo katika Mikoa, Wilaya na Halmashauri zake.


No comments:
Post a Comment