Habari za Punde

Wapinzani Acheni Kumbagua Raza – Gavu

Na Antar Sangali

CHAMA cha Mapinduzi kisema kwamba hakina sera za ubaguzi wa rangi, ukabila, udini wala ujimbo kama vilivyo baadhi ya vyama vya siasa hapa nchini.

Katibu wa Kamati maalum ya NEC wa Itikadi na Uenezi, Issa Haji Gavu alibainisha hayo wakati akimnadi mgombea wa CCM jimbo la Uzini, Mohamed Raza Hassanal Dharamsi, katika kiwanja skuli ya msingi Miwani.

Gavu alisema CCM imerithi sera hizo kutoka vyama vya TANU na ASP ambavyo vilipingana na kuikataa mitazamo hiyo kabla ya uhuru na Mapinduzi ya Zanzibar.


Alifahamisha kuwa vyama hivyo viwili vya ukombozi vyote vilikuwa na wananchama wenye mchanganyiko wa rangi, dini tofauti bila ya kujali kabila na maeneo wanayotoka.

Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi Zanzibar, aliwataka wananchi wa Uzini kupuuza maneno yanayoenezwa na vyama vya upinzani kwamba mgombea wa CCM si mzaliwa wa Uzini na kwamba ni mtanzania mwenye asili ya Asia.

Gavu alisema hakutegemea matamshi hayo kuyasikmia toka kwa viongozi wa vyama vya siasa vilivyo makini ila kwa kufanya hivyo vimetambulika kuwa ni vua kibaguzi.

Akitoa mfano alisema viongozi kama Amir Jamal , Al Noor Kassam, Mohamed Mugheiry, Othman Sharif, Derick Bryson, Dk. Leacky Stearing hawakuwa na asili ya kiafrika ila wamekuwa viongozi kwenye serikali za TANU na ASP.

Gavu aliwataka wananchi wa Uzini kuyapuuza maneno ya vyama hivyo vya upinzani vyenye kupandikiza chuki na ubaguzi na badala yake wavinyime kura kama adhabu kisha wakinyime kura na kuichagua CCM kwa kumpigia kura nyingi Raza kutokana na dhambi za kibaguzi wanazoziendeleza.

Kwa upande wake mgombea wa jimbo la Uzini kwa tiketi ya CCM Mohamed Raza, aliwataka wananchi wa Zanzibar kufanya tafakuri ya kuwakumbuka watu waliopoteza maisha yao kwa kuikomboa Zanzibar Januari 12, 1964.

Raza amesema kabla ya Mapinduzi ya 1964 Zanzibar iligawanywa kwenye makundi ya ubwana,ubwanyenye,ubepari na utwana na kwamba ni sera pekee za ASP ndizo zolizoondosha matabaka hayo.

Aidha mgombea huyo wa CCM amewataka wafanyabiashara walioko nje na ndani wenye asili ya Zanzibar kuendelea kukiunga mkono Chama Cha Mapinduzi huku akisema ndicho kilichotoa fursa na kujenga Umoja.

Akihutubia kwenye mkutano huo, Raza amewaimbisha nyimbo ya ukombozi wa Zanzibar wananchi waliokuwepo mkutanoni kuwakumbuka waliojitoa muhanga na kupoteza maisha yao ili kuikomboa Zanzibar.

Raza aliwasihi wananchi hao kupingana na sera za chama chochote chenye mwelekeo wa kuleta ubaguzi, uhasama na chuki katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Katika mkutano huo, wanachama watano wa CHADEMA kwa hiari zao wamerudisha kadi za chama hicho na kujiunga upya na CCM katika mkutano huo wa hadhara wa kampeni.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.