JUMUIYA ya wasomi wanawake inayosaidia watoto kielimu Tawi la Zanzibar (FAWE Zanzibar), imetakiwa kuhakikisha inawasaidia watoto wa kike kupata msingi mazuri wa kielimu ili wawe wataalamu bora wa baadae.
Akifungua mkutano wa maadhimisho ya kutimia kwa miaka 10 ya kuanzishwa kwa FAWE Zanzibar, Mwenyekiti wa Jumuiya ya ZAYEDESA, Mama Shadya Karume, alisema endapo watasaidiwa watoto wa kike katika suala la elimu wataweza kupunguza majanga mengi ambayo huwakumba yakiwemo mimba za utotoni pamoja na kushiriki katika utumiaji wa dawa za kulevya.
Aidha alifahamisha kuwa wanawake ni nguzo muhimu sana katika kuleta maendeleo, hivyo ni wajibu wa kila mtu kushiriki ipasavyo katika kuhakikisha wanawake wote wanapata elimu iliyo bora ambayo itaweza kumkomboa katika maisha yake na taifa kwa ujumla.
Vile vile ameiomba jumuiya hiyo kuwashajiisha, kuwatunza na kuwashauri vizuri watoto wa kike ili wafanikiwe katika masomo ya sayansi ambayo wengi wao huwa wanashindwa kukosa uelewa mzuri wa faida za masomo hayo.
Nae Mratibu wa FAWE Zanzibar, Asma Ismail, alisema kuwa pamoja na kushajiisha watoto wa kike wanapata elimu bora lakini pia wanafanya kazi ya kuokota watoto wa mitaani waliotoroka na kuwarejesha skuli kuendelea na masomo.
Pia alisema Jumuiya ya FAWE inatoa mafunzo ya ukaguzi kwa wanachama pamoja na utekelezaji wa majukumu yao mbali mbali ya kazi.
FAWE pia ilitoa zawadi kwa washindi wa mashindano ya masomo ya sayansi na wahitimu wa masomo mbali mbali waliofanikiwa kwenda vyuo vikuu kupitia msaada wa Jumuiya ya FAWE.
Aidha Mwenyekiti wa ZAYEDESA, mama Shadya Karume ametoa Shilingi 1,014,000, kukamilisha fedha ambazo zilibakia kukamilisha bajeti ya Mradi wa kuendeleza kimasomo watoto wa kike maskulini Zanzibar unaoendeshwa na FAWE.
Katika maadhimisho hayo pia kulifanyika maonesho ya kimasomo ya kazi mbali mbali za masomo ya sayansi zilizofanywa na wanafunzi.
Hafla hiyo iliyofanyika jana ukumbi wa EACROTANAL Mjini Zanzibar, ilishirikisha wanachama wote wa FAWE Zanzibar.

No comments:
Post a Comment