Na Rajab Mkasaba, Ikulu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, amezitaka Taasisi za mbegu Barani Afrika kuimarisha mbegu za mazao mengine kama vile muhugo na viazi ambazo ni muhimu kwa nchi za Bara hilo kutokana na uwezo wa kustahamili ukame badala ya kuelekeza nguvu kubwa kwenye mbegu za nafaka.
Dk. Shein aliyasema hayo leo katika ufunguzi wa Mkutano wa Mbegu wa Afrika uliofanyika huko katika Hoteli ya Zanzibar Beach Resort, nje kidogo ya mji wa Zanzibar, ambao umehudhuriwa na Wajumbe kutoka zaidi ya nchi 50.
Katika ufunguzi huo, Dk. Shein alisema kuwa Mkutano huo wa 12 unafanyika wakati Tanzania na nchi jirani katika ukanda huu zina matatizo ya kupanda kwa bei za vyakula, athari za mwanguko wa thamani ya fedha na mabadiliko ya hali ya hewa ambazo sababu zote hizo zinatishia juhudi za upatikanaji wa usalama wa chakula.
Kutokana na hali hiyo, Dk. Shein alieleza kuwa Tanzania nayo inahitaji kujitosheleza kwa upatikanaji wa mbegu ili kukidhi mahitaji ya wakulima pamoja na kuuza nje ya nchi kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa chakula na kupunguza umasikini nchini.
Kwa upande wa Zanzibar Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikichukua juhudi kubwa katika juhudi za kutafuta mbegu bora na kukipongeza Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya Kizimbani kwa juhudi zake zilizopelekea upatikanaji wa mbegu bora za muhogo zenye uzalishaji wenye tija na uwezo wa kustahamili ukame.
Dk. Shein, pia, alizipongeza nchi mbali mbali za Afrika kwa juhudi zake inazozichukua katika kuimarisha kilimo cha umwagiliaji maji kama ni njia ya kupambana na changamoto kadhaa zinazoikabili sekta ya kilimo pamoja na kuzipongeza Taasisi Binafsi kwa ushiriki wao imara wa kuendeleza mbegu bora na kuimarisha kilimo Barani Afrika.
Aidha, Katika hotuba yake hiyo Dk. Shein alisema kuwa ili kufikia lengo lililokusudiwa Tanzania imeshachukua hatua za awali zinazohakikisha utekelezaji wa kanuni zilizoweka na zinazofuata na Jumuiya za Kimataifa.
Alisema kuwa mnamo Februari mwaka 2010, Bunge la Tanzania lilipitisha Azimio ambalo linahusu nchi kujiunga na Umoja wa Kitaifa wa Kuhifadhi aina za mimea na hatua za awali zimeshachukuliwa, pamoja na hatua za kufuata taratibu na kanuni zote zilizowekwa na Jumuiya za kudhibiti na kufanya majaribio ya mbegu.
Alieleza kuwa hatua zote hizo zina lengo la kujenga mazingira bora kwa upatikanaji wa mbegu ili kuimarisha sekta ya kilimo hapa nchini.
“Ni matumaini yetu kuwa washiriki wa mkutano huu na Jumuiya nyenginezo za mbegu zitashirikiana na Serikali yetu katika kueneza mbegu bora nchini na katika juhudi zetu za utafiti ili kuleta maendeleo mazuri katika sekta ya kilimo nchini”,alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyengine za Afrika, kilimo ndio msingi mkuu wa uchumi wake kwani sekta hiyo ni tegemeo la ajira kwa silimia 77.5, na tegemeo la upatikanaji wa chakula kwa asilimia 95.
Kwa nafasi hiyo, alieleza kuwa kilimo kina umuhimu wa pekee kwa uchumi wa Taifa sanjari na juhudi za kupunguza umasikini ambapo kwa kutambua mchango wake huo Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zimejiwekea Sera na mikakati ya kuongeza mchango wa sekta ya kilimo kupitia MKUKUTA kwa Tanzania Bara na MKUZA kwa Zanzibar.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alitoa pongezi kwa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Mbegu wa Afrika (AFSTA), kwa uamuzi wao wa kufanya mkutano wao wa 12 hapa Zanzibar.
Alieleza kufurahishwa na malengo ya mkutano huo wa siku nne kwa kujadiliana na kubadilishana uzoefu utakaosaidia kukabiliana na changamoto zinazoibuka katika uzalishaji wa mbegu na sekta ya kilimo kwa ujumla katika bara la Afrika.
Nao, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Profesa Jumanne Maghembe na Kaimu Waziri wa Kilimo na Maliasili, Mhe. Haroun Ali Suleiman walieleza juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapindyuzi Zanzibar katika kuimarisha sekta ya kilimo na mikakati ya uzalishaji wa mbegu nchini.
Rais wa Jumuiya ya AFSTA, Bwana Ennock Chikava nae alieleza kuwa lengo la Jumuiya hiyo ni kuongeza biashara ya mbegu zenye ubora na zinazendana na teknolojia ya kisasa katika nchi za afrika kwa kuwanufaisha wakulima na wajumbe wengineo.
Mapema Dk. Shein aliangalia aina za mbegu zilizotayarishwa na Taasisi mbali mbali za ndani na nje ya Afrika hapo katika ukumbi huo wa Zanzibar Beach Resort.
No comments:
Post a Comment