Mkurugenzi wa hospitali ya Mnazimmoja Dr. Jamal Taibu akitoa maelezo mbele ya Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad kuhusu hali ya utupaji wa taka za hospitali hiyo, wakati Makamu wa Kwanza wa Rais alipotembelea eneo hilo. Katikati ni Waziri wa wa Afya Mhe. Juma Duni Haji.
Na Hassan Hamad OMKR
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, ameuagiza uongozi wa hospitali ya Mnazimmoja kuangalia uwezekano wa kupata makontena ya kuhifadhia taka za hospitali, ili kuepusha athari zinazoweza kujitokeza.
Agizo hilo limekuja kufuatia ziara ya ghafla ya Makamu wa Kwanza wa Rais katika eneo hilo, ambapo ameshuhudia taka za hospitali zikiwa zimewekwa katika eneo la wazi, hali ambayo inaweza kuhatarisha afya za wananchi.
Amesema wakati hospitali ikisubiri kupata mashine mpya ya kuchomea taka baada ya mashine yao kuharibika, ni vyema kutafuta njia muafaka ya kuzihifadhi taka hizo ambapo kwa sasa imeonekana ni kuwa na makontena ya kuhifadhia taka hizo.
Mkurugenzi wa hospitali ya Mnazimmoja Dr. Jamal Taibu amesema wamelazimika kuziweka taka hizo kwenye ndoo na kuzihifadhi katika eneo hilo la hospitali karibu na pwani, baada ya mashine yao kuharibika na kushindwa kupata eneo jengine muafaka la kuziweka.
Awali Makamu wa Kwanza wa Rais alifanya ziara katika Idara ya Mazingira iliyoko maruhubi kuangalia utekelezaji wa majukumu katika Idara hiyo.
Mkurugenzi wa Idara hiyo Bw. Sheha Mjaja amesema pamoja na mambo mengine Idara hiyo inakusuduia kuanzisha operesheni maalum ya kuwaangamiza kunguru weusi, zoezi ambalo linatarajiwa kuanza rasmi mwishoni mwa mwezi huu.
Amesema zoezi hilo litafanywa kwa mashirikiano kati ya taasisi ya uhifadhi wa wanyamapori ya Dar es Salaam na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kupitia Idara ya Mazingira na Idara ya Misitu na maliasili zizorejesheka..
Bw. Mjaja amesema mradi huo unaofadhiliwa na Serikali ya Finland kupitia ubalozi wake uliopo nchini pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, unakusudia kuangamiza kunguru weusi zaidi ya milioni moja.
Hapo jana Makamu wa Kwanza wa Rais alitembelea Tume ya Ukimwi Zanzibar na kuitaka kuongeza juhudi katika kutoa elimu kwa jamii ili kudhibiti maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi nchini.
Amesema licha ya Zanzibar kupata mafanikio mazuri katika kudhibiti kasi ya maambukizi na kubakia kuwa asilimia zero nukta sita (0.6), juhudi zaidi zinahitajika katika kuhakikisha kuwa kiwango hicho kinapungua.
Ameitaka tume hizo kuweka msisitizo katika kutoa elimu hasa kwa vijana katika maeneo yote ya mijini na vijijini, kwa vile wao ndio nguvukazi ya taifa na waathirika wakubwa wa janga hilo, na kwamba iwapo vijana wataendelea kuathirika, taifa linaweza kupata pigo kubwa na kupunguza kasi ya maendeleo.
Makamu wa Kwanza wa Rais pia amehimiza mashirikiano na wadau wengine wakiwemo viongozi wa dini ambao wana nafasi kubwa ya kuwaelimsha wafuasi wao juu ya mapambano dhidi ya janga hilo.
Katika hatua nyengine, Maalim Seif amesema serikali inajiandaa kukabiliana na changamoto za kuiendesha tume hiyo iwapo washirika wa maendeleo watapunguza misaada na ruzuku kwa tume hiyo.
Katibu mtendaji wa Tume hiyo Dr. Omar Makame Shauri amesema miongoni mwa changamoto zinazowakabili ni pamoja na kutegemea zaidi misaada kutoka kwa wafadhili ambayo mara nyingi huchelewa, na hivyo kuchelewasha utekelezaji wa mipango yao.
Dr. Shauri amesema ipo haja kwa serikali kulifikiria kwa umakini suala hilo ili kuepuka athari iwapo wafadhili watashindwa kutoa misaada.
No comments:
Post a Comment