Habari za Punde

Balozi Seif Aonya Tabia ya Viongozi Kuanzisha Migogoro



Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameonya tabia mbaya inayofanywa na baadhi ya Viongozi kwa kuanzisha migogoro inayoweza kusababisha madhara kati ya Wawekezaji na Wananchi hapa Nchini.

Onyo hilo amelitoa mara baada ya kufanya ziara Maalum ya kukagua Mashamba ya Miwa ambayo baadhi yake yamelimwa Mpunga kinyume na Utaratibu wa makubaliano baina ya Uongozi wa Wilaya ya Kaskazini B na Kiwanda cha Sukari Mahonda.

Balozi Seif alisema ushawishi Unaofanywa na Baadhi ya Viongozi hao kuwahamasisha Wakulima kuendeleza kilimo katika mashamba hayo ni kukaribisha migogoro kati ya Muwekezaji huyo na Wananchi ambao unaweza kuwepukwa.

Alisema Jamii inapaswa kuheshimu maamuzi ya Serikali wakati inapopanga utaratibu wa Maendeleo hasa inapotiliana saini mikataba na Wawezekaji katika kuanzisha Miradi ya Kiuchumi.


“ Inasikitisha kuona Wananchi wamepotoshwa kulima katika maeneo haya bila ya kuzingatia utaratibu na busara”. Alisema Balozi Seif.

Balozi Seif aliupongeza Uongozi wa Kiwanda cha Sukari Mahonda kwa kushirikiana na Serikali ya Wilaya ya Kaskazini B katika jitihada za kuwaazima Wakulima Hekta zaidi ya 2000 ili kuendeleza Kilimo cha Mpunga.
Alisema Imani hiyo ya Uongozi wa Kiwanda cha sukari inapaswa kushukuriwa kwa vile haukulazimika kutoa fursa hiyo kutokana na Mkataba wake na Serikali.

Mapema Mkurugenzi wa Operesheni wa Kiwanda hicho Bwana Hilary Njau alimueleza Balozi Seif kwamba uvamizi pamoja na utiaji moto wa mashamba ya miwa umekuwa ni tatizo sugu la muda mrefu.

Bwana Njau aliiomba Serikali kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo ambalo limekuwa likirejesha nyuma nguvu zao za uwekezaji.Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi baadaye alilikagua Eneo linalokusudiwa kujengwa Msikiti na Chuo cha Kiislamu liliopo Muyuni Matemwe wilaya ya Kaskazini A.

Balozi Seif akiwa pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM alilikagua Jengo jipya la Maskani ya Wazee wa CCM ya Tungalipo liliopo Pwani Mchangani.

Akizungumza na Wazee hao Balozi Seif alisema Chama cha Mapinduzi kinathamini mchango wa Wazee wakati wa kupigania Uhuru wa Taifa hili.

Balozi Seif ambae aliahidi kusaidia gharama za uwezekaji wa Maskani hiyo alisema CCM bado inaendelea kuwa Chama makini kutokana na kupata ridhaa ya Wananchi kuiendesha Serikali.

Akilikagua Shamba lililokuwa la Chama cha Afro Shirazy Party na sasa CCM liliopo Kirombero Balozi Seif Amewaasa Viongozi kuwa waangalifu wa kusimamia mali za Chama.

Alisema mali za Chama lazima ziheshimiwe na kushauri kufanywa kampeni maalum ya upandaji wa miti mchanganyiko ili kuongeza mapato ya Chama.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
7/3/2012.


1 comment:

  1. viwanda vyote vya nchi vinatakiwa virudi kwenye uzalishaji, tuache siasa kwa muda.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.