Habari za Punde

Hii ndiyo Zanzibar tunayoitaka?

Na Salim Said Salim

ZANZIBAR ni njema…atakaye aje. Huu ni usemi maarufu wa wahenga wa Visiwani ambao umekuwa na lengo la kuwaonyesha majirani zake na ulimwengu kwa ujumla kwamba Zanzibar hakuna matatizo ya kimaisha na kwamba watu wake ni wema, wakarimu na rahimu na atakaye kuja kuishi au kutembelea Zanzibar anakaribishwa kwa mikono miwili na moyo mkunjufu.

Kumbukumbu zinaonyesha jamii yoyote ile duniani, bila ya kujali imani zao, tofauti za dini au makabila, siku zote huwa inapendelea na kuweka sheria zitazohakikisha mila, utamaduni na desturi za watu wake zinaendelezwa na mtu yoyote yule, awe mwenyeji au mgeni, anayezibughudhi, kuzikejeli au kuzidharau huonekana hana nia njema na jamii hiyo.


Ni kweli katika zama hizi za utandawazi dunia imeshuhudia mabadiliko mengi ya kijamii na maisha kwa jumla. Jambo ambalo miaka ya nyuma hapa kwetu lilionekana si la kawaida, kama mwanamume kuvaa herini au kidani, limekuwa likikubalika siku hizi. Wapo walioipokea hali hiyo kwa furaha na wapo walioiridhia kwa shingo upande, lakini hiyo ndio hali ya dunia ya leo.

Mambo kama haya ndiyo yalisabisha Waswahili wa kale kusema kiingiacho mjini si haramu, lakini wapo watu leo wanaotofautiana na kauli hii na kusema pia si kila kinachoingia mjini ni halali.

Katika mambo ambayo watu wa Zanzibar wamekuwa wakiyajali sana na kutoyafanyia mzaha ni mavazi. Kwenda uchi au nusu uchi hadharani ni mambo ambayo watu wa Visiwani wamekuwa hawayakubali na hata anapotokea mtu mwenye matatizo ya akili anafanya hivyo watu hujitolea kumsitiri kwa kumvisha nguo. Hayo ndio maisha ya watu wa Zanzibar.

Visiwa hivi vimekuwa kwa muda mrefu na sheria zake za mavazi. Sheria hizi izlitiliwa mkazo baada ya Mapinduzi ya 1964 ambapo hata watalii waliokuja Zanzibar wakiwa na mavazi ambayo kwa mila, silka, desturi na utamadini wa Zanzibar hayakubaliki walitakiwa kuchagua – kununua doti ya kanga au kitenge na kufunika sehemu ambazo watu wa Visiwani wanaona hazifai kuanikwa hadharani.

Rais wa Kwanza wa Zanzibar, hayati mzee Abeid Aman Karume, aliwahi kusema: “Fedha za kigeni za watalii hazina thamani inayozidi mila na desturi zetu. Akitaka kwenda mtu uchi aende kwao si hapa kwetu Zanzibar”.

Mwaka 1965, aliyekuwa Rais wa Liberia, William Tubman, alipokuwa amepanga kufanya ziara ya Zanzibar alitaka watu wote watakaokwenda Uwanja wa Ndege wa Zanzibar kumpokea wavae suti. marehemu mzee Karume alikasirishwa na maelekzo yale na yeye alimpelekea salamu Tubman kumwambia kuwa mgeni yeyote anayefika Zanzibar kwa matembezi ya kiserikali, basi lazima avae kanzu, koti, kofia na viatu vya makbadhi.

Matokeo yake baada ya mazungumzo marefu ya kidiplomasia, Tubman alikuja Zanzibar akiwa amevaa suti yake na watu waliompokea walivaa kanzu, koti, kofia na makbadhi na alipewa vazi hilo kama zawadi alipoondoka.

Hili lilikuwa somo kuwa watu wa Zanzibar hawakuwa tayari kuona wageni wanachezea utamaduni wao.

Wakati ule watalii walielezwa tokea huko kwao kabla ya kufanya safari ya kuja Zanzibar aina ya mavazi ambayo wanatakiwa wavae wanapokuwapo Visiwani na kuambiwa kuwa kutotii maelekezo hayo ni kosa la jinai. Wapo watalii waliojaribu kukejeli maelekezo hayo na matokeo yake ni kusukumwa jela kwa wiki kadha na kunyolewa vipara. Hili lilikuwa fundisho kwa wengine.

Hivi sasa sheria hizi bado zipo, yaani hazijafutwa. Lakini kinachoonekana ni kufumbiwa macho na kupelekea watu kulalalama pembeni na hadharani kwamba utalii unavuruga mila, utamaduni na desturi walizorithi watu wa Zanzibar kutoka kwa wazee wao.

Ni kawaida siku hizi kuona kundi la watalii wanatembea na vichupi katika Soko Kuu la Zanzibar na kuwaacha watu wakitikisa vichwa na kujiuliza: Hii ndiyo Zanzibar tunayoitaka? Huko vijijini mambo hayasemeki.

Watalii wanaofikia katika hoteli za fukwe za bahari huenda vijijini kutembea wakiwa wamevaa bikini (vazi la chupi na sidiria) na kusababisha vizee kukimbilia nyumbani kwao kujificha kwa vile macho yao hayawezi kuona aibu ile.

Ni kweli utalii kwa hivi sasa unaiingizia Zanzibar asilimia 73 ya pato lake la fedha za kigeni na kuchangia wastani wa asilimia 25 ya pato la taifa kila mwaka. Hapa suala linalofaa kujiuliza je, ni haki na sawa kwa fedha za kigeni ziruhusiwe kuvuruga utamaduni, mila na desturi za watu wa Zanzibar?

Ni vizuri kwa wahusika katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuitafakari hali hii kwa sababu kuna manung’uniko ya wananchi juu ya watalii kwenda uchi au nusu uchi hadharani, mambo ambayo hata huko kwao hawayafanyi, yamekuwa makubwa na yanawaudhi watu.

Hivi sasa watu wanalalamika na wanaonekana kuvumilia mwenendo huu kwa unyonge, lakini ipo hatari ya kutokea watu wakashawishi vijana kuonyesha hasira zao na matokeo yake kuwa mabaya. Ni kweli watu wanao uhuru wa mavazi, lakini si kwenda uchi hadharani.

Inawezekana wakatokea wale ambao watasema huwezi kuwachagulia watu aina ya nguo za kuvaa, lakini hapa tukumbuke kuwa hao Wazungu wanaokuja kwetu na kutembea nusu uchi pia wanazo sheria za mavazi huko kwao.

Miongoni mwao ni kukataza wanafunzi wasivaie hijabu wanapokuwa shule na wale wanaojifunika gubigubi au kuvaa “Ninja” kutoruhusiwa sehemu nyeti, kama mabenki.

Sasa kama watu wengine wanaweza kuwa na sheria za mavazi na kuambiwa lengo lake ni kulinda usalama wao, kwa nini Zanzibar ione tabu kuendelea na kuwa na sheria za mavazi za kulinda mila, utamaduni na desturi za watu wake?

Hili ni suala nyeti ambalo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haistahili kulipuuza. Ni ukweli usiokuwa na ubishi kuwa zaidi ya asilimia 95 ya watu wa Zanzibar ni Waislamu na imani ya dini yao ndiyo siku zote imekuwa mhimili mkuu wa sheria za nchi na mwenendo wa maisha yao. Utanda wazi usiwe sababu ya kuvuruga mwenendo wao wa maisha.

Watalii wanaweza kuvaa hizo bikini zao vyumbani mwao, kwenye ufukwe wa bahari au wanapokuwa kwenye maeneo ya hoteli walizofikia, lakini si kwenda na vivazi hivyo sokoni au mitaani na kuwaudhi watu ambao hawataki mila na utamaduni wao kuvurugwa na wageni wala wenyeji.

Watu huringia mila na tamaduni zao na Wazanzibari wanayo haki ya kuringia mwenendo wa maisha waliorithi kutoka kwa wazee wao.

Kama wengine watasema watu wa Visiwani hawajaendelea, ieleweke kuwa kwa watu wa Zanzibar maendelo kwao wao si kwa mwanamume kuvaa herini au kidani, watu wa jinsia moja kufunga ndoa au mtu kwenda uchi hadharani.

Ni matumaini yangu kuwa kiu ya kupata fedha za kigeni kutokana na sekta ya utalii haitakuwa sababu ya kuvuruga mila na utamaduni wa watu wa Visiwani.

Zanzibar inaweza kubakia kuwa ni njema na atakae aje, lakini aje kwa heshima, wema na hisani na anapaswa kutodharau mila, utamaduni na desturi za watu wake.

Chanzo: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.