Na Mwantanga Ame
WANANCHI wametakiwa kuwajibika katika kufanikisha mpango wa upatikanaji maji safi na salama nchini, pamoja na kuifanya huduma hiyo kuimarika na kuwa endelevu.
Wito huo umetolewa jana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, alipohutubia wananchi katika kilele cha wiki ya maji huko tangi la maji Saateni Mjini Zanzibar.
Dk.Shein ameeleza kwamba ili suala la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama nchini liweze kufanikiwa wananchi wote wanahitaji kuwajibika na kuelewa kuwa hilo ni jukumu lao kwa kushirikiana na serikali yao.
Alisema kila mmoja anawajibika kuwa mlinzi wa vianzio na miundombinu ya maji, wananchi waache tabia ya kujenga katika vianzio vya maji, pamoja na kutumiwa vyema maji, huku akiwasisitiza wananchi kutoa taarifa za maharibiko ya miundombinu ya maji katika vyombo vinavyohusika kwa haraka.
Alisema ingawa kuna faraja ya kuwepo kwa idadi ya watu bilioni 2,000,000,000 wameweza kupatiwa huduma ya maji kwa asilimia 89 ambayo ni sawa na bilioni 6.1 hadi kufikia mwaka 2010, bado kuna watu zaidi ya milioni 800 wengi wao wakiwa Kusini ya Jangwa la Sahara ambao wanahitaji kusaidiwa kupata huduma hiyo.
Alisema Serikali ya Zanzibar itaendelea na mikakati yake kuhakikisha wananchi wa Zanzibar wanapata maji safi na salama, ikizingatiwa umuhimu wa maji kwa uhai wa viumbe vyote.
Katika kufanikisha hilo, Dk.Shein amesema tayari serikali imechukua mkopo wa shilingi bilioni 33 katika Benki ya Maendeleo ya Afrika, kugharamia kupatikana kwa maji safi ambazo zitatumika kwa ajili ya uimarishaji wa miundombinu, ujenzi wa visima na kuijengea uwezo Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA).
Alisema serikali inalazimika kuwapatia maji wananchi kwani ni moja ya jambo la msingi katika masuala ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii ambapo huweza kuwapa watoto hasa wa vijijini kujishughulisha na masomo yao, kuimarisha kilimo, na kuiwezesha jamii kujenga afya bora.
Dk.Shein aliwataka wananchi kujenga tabia ya kuchangia katika maendeleo ya nchi na yao binafsi, kwani hiyo ndiyo njia muafaka ya kufikiwa maendeleo endelevu nchini.
Suala la kuzingatiwa Dk. Shein, alisema ni kwa wananchi wenyewe kuacha tabia ya kuilaumu serikali kwa kila kasoro inayojitokeza kwenye jamii, na badala yake wajijengee uwezo wa kuwabaini wanaoharibu miundombinu ya maji katika maeneo wanayoishi kuviripoti vitendo hivyo mapema.
Aidha, Dk. Shein alionya tabia ya kujenga karibu na kwenye vianzio vya maji kwani kufanya hivyo ni moja ya hatari inayopunguza upatikanaji wa huduma ya maji.
Rais Dk. Shein, aliitaka jamii kulipia huduma ya maji kwa wale wote wanaoipata, ili kuweza kuchangia gharama za usambazaji maji hadi kufika katika maeneo yao, huku akielekeza kuwa wasiopata maji wasilazimishwe kulipa hadi watapopatiwa huduma hiyo.
Kabla ya kuhutubia, Dk.Shein alizindua maonesho ya huduma za maji safi na salama Zanzibar, ambayo yanaonesha historia hadi hali ilivyo sasa na kuwataka wananchi kufika katika eneo hilo kujionea maonesho hayo ambayo ni hazina kwa Zanzibar.
“Niliyoyaona katika maonesho haya ni makubwa, kwani ni ya kihistoria na mengine huwezi kuyaona katika nchi nyengine ila Zanzibar, ni vyema ZAWA mkaona namna ya kuyatunza li vizazi vijavyo vifaidike kwa historia hii nzuri” alisisitiza Dk.Shein.
Mapema Dk. Shein alimkabidhi mfanyakazi wa Mamlaka hiyo Mohammed Ali Habsi cheti cha kuwa mtumishi bora alieitumikia Idara hiyo tangu 1964 .
Waziri wa Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, Ali Juma Shamuhuna alisema licha ya serikali kufanya jitihada mbali mbali lakini kuna baadhi ya watu wamekuwa wakifanya mambo yanayosikitisha kwa kuvuruga mfumo wa maji kwa kujenga karibu na vianzio vya maji.
Alisema hali hiyo imekuwa ikisababisha kuwepo kwa uhaba wa upatikanaji wa huduma ya maji kwa uhakika kutokana na kupungua kwa kasi kufuatia uharibifu mkubwa wa vianzio, pamoja na ukataji ovyo miti.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, Mwalimu Ali Mwalimu, akitoa maelezo ya kitaalamu alisema serikali katika kuhakikisha inawapatia huduma ya maji safi haijawahi kuzembea wala kusinzia lakini bado wanakabiliwa na changamoto mbali mbali za kimaendeleo.
Alizitaja kati ya changamoto hizo ni kupungua kwa maji kwenye chemchem, kuharibika vianzio vya maji huku kukiwa na ongezeko la idadi ya watu na uchakavu wa miundombinu ya kusambazia huduma hiyo.
Katika sherehe za wiki ya maji hapo juzi, Dk.Shein aliwaahidi wananchi wa Zanzibar kuwa Serikali itaendelea kuwapatia huduma ya maji safi na salama kwa vile ni haki yao.
Dk. Shein aliyasema hayo alipozindua mradi wa maji wa Mfenesini, kituo cha maji cha Selemu, wilaya ya Magharibi Mjini Unguja.
Alisema sera ya serikali ni kuona wananchi wanapata maji safi na salama na ndio maana imeamua kufanya kila jitihada kuona haki hiyo wananchi inawafikia kutokana na umuhimu wake.
Alisema kazi hiyo serikali imekuwa ikiifanya kwa kutumia nguvu zake pamoja na wananchi huku wakishirikiana na taasisi za kimataifa ambazo huamua kujitolea kuisaidia zanzibar.
Alisema malengo ya Mapinduzi ya 1964, ni kuwapatia huduma bora wananchi na serikali ya awamu ya saba itahakikisha inaendeleza dhamira hiyo.
Dk.Shein alisema wataalamu wa sayansi wanatufahamisha kuwa uwezekano wa kuwepo kwa maisha katika sayari nyengine zilizotuzunguka ni ndogo sana kwani hadi sasa hawajabaini kuwepo hata matone madogo madogo ya maji katika sayari hizo.
Kutokana a hali hiyo, aliwataka wananchi kuhakikisha wanatumia vyema raslimali hiyo huku wakithamini mchango wa wanaojitolea kustawisha upatikanaji wa maji.
Alisema kitendo cha mashirika ya CHANGAMOTO LPF, ANGOZA, ZAFFID, ACRA ya Italia na FAI kuamua kujitolea kufanikisha mradi huo, wananchi watapaswa kuithamini kwa kutumia vizuri nishati hiyo pamoja na kutunza vyanzo vya maji na kuacha kufanya uharibifu wa miundombinu ya maji.
Dk. Shein aliyapongeza mashirika hayo kwa kufanikisha mradi huo baada ya Jumuiya ya Ulaya kutoa asilimia 71.5 ya fedha za kutekeleza mradi huo ambao umetumia bilioni 1.8 na utaweza kuwatumikia wanannchi 46,000 katika shehia 18 za Majimbo ya Kitope, Bumbwini na Mfenesini, na kuahidi kushirikiana nayo
Mapema Mwakilishi wa ACRA, akitoa maelezo yake Alesia Lonbardo shirika lao litaendela kuisaidia Zanzibar kwa kuyapatia ufumbuzi matatizo ya maji.
Alisema Umoja wa mataifa kupitia mpango wake wa Milenia tayari imetangaza kufanikiwa kuimarisha huduma ya maji katika maeneo mbali mbali duniani.
Alisema katika mradi huo Jumuiya ya Ulaya, imechangia EURO 750,000, SMZ kupitia ZAWA imechangia 105,000, Fondazione Renato Grandi Euro 80,000, Briaze Acque Spa wamechangia shilingi 50,000.
Mapema Dk. Shein, alipokea taarifa ya Mkoa wa Mjini, ambayo imeelezea mambo mbali mbali ikiwa pamoja hali ya usalama ya mkoa ambapo ilieleza iko vizuri kutokana na mfumo unaoendelea wa serikali ya umoja wa kitaifa.
Aidha, taarifa hiyo imeeleza juu ya kuwapo kwa changamoto mbali mbali ambazo tayari serikali imeshaandaa mipango juu ya namna ya kukabiliana nazo ikiwemo ya dawa za kulevya.
No comments:
Post a Comment