Joseph Ngilisho, ARUSHA
MWENYEKITI wa kamati ya Bunge ya Hesabu za serikali za Mitaa (ALAT), Augustine Mrema ameitaka wizara ya TAMISEMI kuacha tabia ya kuwakaimisha kwa muda mrefu wakurugenzi na wakuu katika halmashauri, kwani kufanya hivyo ni kukaribisha wizi.
Mrema alieleza hayo jana kwenye majumuisho baada ya kamati hiyo kufanya ziara ya siku tatu mkoani Arusha, ambapo alisema pia tabia hiyo inapunguza morali kwa watendaji.
Kamati hiyo ambayo ilitembelea Halmashauri za Monduli, Arusha Vijijini na Manispaa ya Arusha, alisema watendaji wengi katika halmashauri hizo ni watu wasiojua kitu.
Mwenyekiti huyo alisema kutokana na baadhi ya watendaji hao kutoelewa kile wanachokifanya haitarajiwi na kwamwe hawawezi kuzimarisha halmashauri na miradi mbalimbali ya maendeleo.
Aliongeza kuwa, kitendo cha wakuu wa Idara kukaimu nafasi zisizo zao kwa kipindi kirefu, kinazorotesha utendaji kazi katika Idara na wengi wao wanakuwa hawana utaalamu wa kile wanachofanya.
Mrema alisema kuwa, katika maeneo mengi waliyopitia wamekuta nafasi nyingi zinakaimiwa hali ambayo inakuwa ni vigumu kupata majibu sahihi pale wanapowahoji kutaka taarifa mbali mbali za kimaendeleo pamoja na utekelezaji wa miradi.
“Ninachowashauri TAMISEMI kama wameweza kumweka mtu akakaimu hadi miaka mitano hadi sita basi ni vizuri wapewe ajira kabisa kama ana viwango vya kutosheleza kama hawezi basi watafute mtu atakayeweza kushikilia nafasi”, alisema Mrema.
Akitoa mfano Mrema alisema katika halmashauri ya Monduli jumla ya wakuu 12 wa Idara mbali mbali wanakaimu nafasi hali ambayo iliwashangawa kwani walipokuwa wakiwahoji kuhusiana na utekelezaji wa miradi hawakua na majibu bali kuishia kusema wao wanakaimu tu.
Alisema nafasi nyingi kukaimiwa kuliifanya kamati yake kukosa taarifa sahihi kuhusiana na miradi mbali mbali inayotekelezwa na halmashauri hizo na kubaini kuwa fedha za miradi wanazoidhinisha haziendani na kiwango cha kilichopangwa.
Aliongeza kuwa, kumekuwepo na uwajibikaji mdogo katika miradi mbalimbali ya halmashauri zote ambapo miradi mingi haiendani na fedha zilizotolewa kwani haijiridhishi, hivyo juhudi zinahitajika kuhakikisha miradi hiyo inafuatiliwa na kufanyiwakazi kwa upya.
Mrema alimwagiza pia Mkuu wa mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo kuhakikisha anafuatilia kwa kina halmashauri hizo kwani nyingi zina matatizo mkubwa sana na hakuna mtu yeyote anayefika kuwasemea na wamefika mahali ambapo kwa sas ahivi wamejisahahu wanafanya vitu kwa kutaka wao wenyewe.
No comments:
Post a Comment