Wachezaji, makocha wafungiwa, wapigwa faini kwa vurugu
Na Haji Nassor, Pemba
RUNGU la adhabu limeishukia timu ya soka ya KMKM kufuatia vurugu zilizotokea Machi 20, 2012 ilipocheza na Super Falcon katika ligi kuu ya Zanzibar kwenye uwanja wa Gombani.
Katika vurugu hizo zilizozimwa na askari wa kikosi cha kutuliza ghasia cha jeshi la Polisi, wachezaji wa timu hiyo walimsulubu muamuzi Hassan Gerei kwa kumshushia kipigo na kusababisha mchezo kuvunjika katika dakika ya 76, timu hizo zikiwa sare 1-1.
Kwa mujibu wa barua ya Chama cha Soka Zanzibar, ofisi ya Pemba, iliyoandikwa jana Machi 22, 2012 ikiwa na kumbukumbu namba ZFA/T/BAF/VOL V/P/275, iliyosainiwa na Msaidizi Katibu Mkuu Abdallah Suleiman Sharif, kamati tendaji imebaini kuhusika kwa KMKM katika kadhia nzima.
Barua hiyo imewataja wachezaji Mudrik Muhibu Abdallah, Khalid Khamis Juma na Juma Mbwana Faki, kuwa ndio waliompiga muamuzi huyo na kumsababishia majeraha ya kichwa na jicho.
Aidha imeelezwa kuwa, makocha wa timu hiyo walikuwa chanzo cha ghasia hizo zilizopelekea mchezo kuvunjika kabla ya wakati wake.
Kocha Msaidizi Ali Vuai Shein, ambaye awali alikwishaondoshwa katika benchi na kuamriwa kupanda jukwaani kutokana na kutoa lugha chafu kwa waamuzi, alidaiwa kuteremka na kushiriki kumpiga Gerei pamoja na kuhamasisha wachezaji kufanya kitendo hicho.
Naye Kocha Mkuu Ali Bushiri, alidaiwa kuwa tangu mchezo ulipoanza alikuwa akitoa maneno machafu dhidi ya waamuzi, kuvuta sigara licha ya kuonywa mara kadhaa pamoja na kushajiisha kupigwa muamuzi kwa vile hakuchukua hatua ya kuwakataza wachezaji wake wasifanye hivyo.
Aidha, wachezaji Khamis Ali na Ventras John wamedaiwa kushirikiana na Bushiri kuendeleza fujo, licha ya kuaswa, na kutokana na vitendo hivyo vya utovu wa nidhamu, wanandinga hao wamefungiwa kutokucheza mechi tatu za ligi kuu kuanzia tarehe ya barua hiyo, pamoja na kupigwa faini ya shilingi laki moja kila mmoja.
Wachezaji wengine, Mudrik Muhibu na Khalid Juma, wamefungiwa kutokushiriki ligi kuu kwa muda wa miezi sita, na pia walipe faini ya shilingi laki moja kila mmoja, huku Kocha Msaidizi Shein, akitakiwa asitie mguu katika mechi za ligi kuu wala kufundisha kwa kipindi cha miezi sita na faini ya shilingi laki moja.
Naye Ali Bushiri ametakiwa asikalie benchi la timu yake katika mechi mbili zitakazofuata, sambamba na faini ya shilingi laki mbili, huku mmoja wa viongozi wa timu hiyo, Hassan Ameir akipewa onyo kali, ambapo Meneja Said Ali Mfaume amepongezwa kwa kujaribu kuwazuia wachezaji na viongozi wenzake wasimtwange muamuzi.
Kutokana na kadhia hiyo, kamati tendaji ya ZFA Taifa Pemba imeibarikia ushindi wa mabao mawili na pointi tatu timu ya Super Falcon.
Kama wachezaji wa KMKM ni askari wa KMKM basi mimi sishangai kuwa wamepiga muamuzi wa mchezo wa mpira. KMKM wamewahi kuripotiwa siku za nyuma kupiga watu bila kosa. Nafikiri wanajiona wako juu ya sheria. Pia tabia hii ya kupigwa muamuzi ni kitendo cha aibu mpirani. Mie nahisi wangeongezewa adhabu.
ReplyDelete