Habari za Punde

KMKM Yazishika Ngarawa za Mundu

Na Mwajuma Juma

WAVUVI wa nguru kutoka kijiji cha Nungwi timu ya Mundu, wameshindwa kuvua katika bahari ya Kibweni baada ya ngaraza zao kuzamishwa na mabaharia wa KMKM walipofungwa goli 1-0 kwenye mchezo wa ligi kuu ya soka Zanzibar.

Mchezo huo uliopigwa juzi katika uwanja wa Mao Dzedong, ulikuwa na ushindani na mkali na kutoa burudani murua kwa mashabiki wachache waliofika kuangalia pambano hilo.

Licha ya mashambulizi mengi ya kila upande, miamba hiyo ilikwenda mapumziko bila yeyote kuziona nyavu za mwenzake.


Hata hivyo, kipindi cha pili, timu zote zilirekebisha makosa yao na kufanya mabadiliko kadhaa ambayo yaliinufaisha zaidi KMKM iliyomudu kujipatia bao pekee katika dakika ya 75 lililonasishwa kimiani na Vuai Juma.

Matokeo hayo, yamewafanya washika magendo hao wanaonolewa na kocha Ali Bushiri kufikisha pointi 22 na kushika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo, nyuma ya vinara Miembeni United yenye pointi 23.

Patashika ya ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena leo uwanjani hapo, ambapo maafande wa Polisi watakuwa kibaruani dhidi ya Jamhuri kutoka Pemba.

Na katika mchezo wa ligi daraja la pili Taifa ambao pia ulichezwa uwanjani Mao wakati wa saa 8;00 mchana, wanajeshi wa JWTZ timu ya Kipanga, waliweza kuisambaratisha Eleven Fighters ya Bububu kwa mizinga 4-0.
Mabao ya wanaulinzi hao yalipachikwa nyavuni na Ramadhan Ajali, Jecha Simai pamoja na Juma Khamis.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.