Habari za Punde

Mswada mfuko wa Jimbo kuwasilishwa Barazani Baraza la Wawakilishi kuanza leo

Na Mwantanga Ame

VIONGOZI wa majimbo wanatarajia kupata afueni baada ya serikali kuandaa mpango wa kuwasilisha mswada wa sheria wa kuanzishwa kwa mfuko wa Jimbo katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoanza leo Mjini Zanzibar.

Hatua hiyo ya serikali itaichukua baada ya kuwasilisha mswada wa sheria wa kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo Zanzibar, na mambo mengineyo ambao tayari umewasilishwa kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Muda mrefu Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, waliiomba serikali kuanzisha mfuko huo kwa lengo la kuwawezesha kupata fedha zitazowasaidia kuyahudumia majimbo yao.

Mfumo wanaoutumia hivi sasa wamekuwa wakipatiwa fedha hizo kupitia Wizara ya fedha ambapo huingiziwa shilingi milioni 5,000,000 kwa kipindi maalum baada ya kuainisha miradi ya maendeleo wanayotaka kuitekeleza majimboni mwao ambapo husimamiwa na serikali kuu.

Tayari mfuko kama huo umeanzishwa kwa Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo wamekuwa wakipatiwa fedha zinazotumika kwa ajili ya shughuli za maendeleo majimboni mwao.

Kutokana na kuwepo kwa hali hiyo serikali imeamua kuweka Mswada huo ambapo umeeleza lengo lake ni kutunga sheria itayoruhusu kuanzishwa kwa mfuko wa Maendeleo ya Jimbo wa Zanzibar, kwa ajili ya kurahisisha maendeleo katika majimbo ya hapa nchini.

Chini ya Mswada huo sheria hiyo ikiwa itapitishwa na kuwekewa saini na Rais, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi watapaswa kuamua hatima ya maendeleo ya majimbo yao kwa kushiriki katika uanzishaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa mujibu wa vipaumbele vyao.

Aidha, Mswada huo unakusudia kuweka mazingira endelevu zaidi kwa majimbo yote ya Zanzibar kuwajibika katika kupambana na umasikini na kuleta maendeleo katika majimbo yao.

Eneo jengine ambalo mswada huo umelenga ni namna ya kuimarisha maendeleo katika majimbo yote ya Zanzibar katika hali iliyo sawa.

Pia mswada huo unaotarajiwa kuwasilishwa na Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammmed Aboud Mohammed, umeeleza utatoa adhabu kwa mtu yoyote ataetumia vibaya fedha au mali za mfuko huo kinyume cha matakwa ya sheria hiyo kwa vile atakuwa ametenda kosa.

Adhabu, iliyowekwa katika mswada huo ni kupigwa faini ya shilingi milioni 10,000,000 na si zaidi ya milioni 20,000,000 au kifungo kisichopungua miaka mitano ama adhabu zote mbili.

Adhabu nyengine ambayo imetajwa katika mswada huo ni ya kulifa faini ya shilingi 5000,000 na sio zaidi ya shilingi milioni 2,000,000 au adhabu zote mbili.

Mswada mwengine unaotarajiwa kuwasilishwa katika kikao hicho ni wa kufuta sheria namba 5, ya mwaka 1989 ya Tume ya Mipango na kutunga sheria mpaya kwa ajili ya uendeshaji wa Tume ya Mipango ya Zanzibar kazi zake, uwezo wake na mambo mengine yanayohusiana na hayo.

Mswada mwengine utawasilishwa na Waziri wa Nchi Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mwinyihaji Makame, utahusu sheria ya maslahi ya viongozi wa kisiasa ya mwaka 2012.

Waziri wa Kilimo na Mali Asili, Mansour Yussuf Himid, nae anatarajiwa kuwasilisha mswada wa sheria ya kuanzisha taasisi ya Utafiti wa Kilimo na mambo mengineyo yanayohusiana na hayo na mswada wa sheria ya marekebisho sheria ya Utalii namba 6, ya mwaka 2009.

Pia kikao hicho kitafanya marekebisho ya sheria mbali mbali kwa kuweka masharti bora ndani yake, na mswaada wa sheria ya kuanzisha Bodi ya vipimo na tathmini ya Elimu Zanzibar na mambo mengineyo yanayohusiana na hayo.

Mambo mengine ambayo yanatarajiwa kutokea ndani ya kikao hicho ni kwa Baraza hilo kupokea kauli za Mawaziri kwa kuwasilisha ripoti za Uchunguzi baada ya hapo awali Wajumbe wa Baraza hilo kuliomba Baraza kuunda Tume za kuzichunguza baadhi ya taasisi zake, huku nyengine zizotolewa hoja binafsi.

Ripoti ambazo zinatarajiwa kuwasilishwa katika kikao hicho, itayohusu taarifa ya Eneo la Bahari la Ukanda wa Kiuchumi, ambapo Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, Ali Juma Shamhuna atawasilisha maelezo yake juu ya suala hilo, baada ya Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe Ismail Jussa Ladhu, kikao kilichopita kuwasilisha hoja binafsi.

Suali nyengine ya serikali inatarajiwa kutolewa na Waziri wa Nchi Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mwinyihaji Makame, atayewasilisha ripoti inalolihisu Baraza la Manispaa baada ya Wajumbe wa Baraza hilo kutaka kuundwa tume ya kuchunguza mikataba iliyofungwa na taasisi hiyo.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ramadhan Abdalla Shaaban, anatarajiwa nae kutoa kauli ya serikali juu ya suala la Mikopo ya Elimu ya Juu baada ya kikao vilivyopita Mwakilishi wa Jimbo la Kwamtipura Hamza Hassan Juma kuwasilisha hoja binafsi juu ya suala hilo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Baraza la Wawakilishi pia kikao hicho kinatarajia kupokea hoja binafsi juu matatizo yaliomo ndani ya shirika la umeme itayowasilishwa na Mwakilishi wa Kiwani Hija Hassan Hija ambaye anataratijiwa kuliomba baraza hilo kuunda kamati teule ya kulichunguza shirika hilo.

Kazi nyengine ambazo zinatarajiwa kufanywa na kikao hicho ni pamoja na kupokea ripoti za kamati teule za kudumu za baraza la Wawakilishi na Kamati ya kudumu ya Baraza hilo.

Spika wa Baraza la Wawkilishi Pandu Ameir Kificho, katika kikao hicho anatarajiwa kumlisha kiapo Mwakilishi wa Jimbo la Uzini, Mohammedraza Hassanali Mohamedali Dharamsi, alieshinda uchaguzi katika Jimbo hilo.

Jumla ya maswali 153 yanatarajiwa kuulizwa na Wajumbe hao na kupatiwa majibu kutoka kwa watendaji wakuu wa serikali amabapo kikao hicho kinatarajiwa kufanyika ndani ya kipindi cha wiki mbili.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.