Na Khamisuu Abdallah
JESHI la Polisi mkoa wa Mjini Unguja linamsaka kijana Himirian Evon Himirian (25), kwa tuhuma za kumiliki bangi kinyume na sheria.
Kwa mujibu wa Kamanda mkoa wa mjini Magharibi Kamishna Msaidizi wa Polisi, Aziz Juma Mohammed alisema kijana huyo mara baada ya kupata taarifa kwamba atakamatwa alifanikiwa kuroroka na kuacha mzigo wake.
Mtuhumiwa huyo anadaiwa kupatikana na mifuko 7 mikubwa yenye majani makavu yanayosadikiwa kuwa ni bangi ambayo aliyopatikana nayo katika maeneo anayoishi ya Maungani kichaka punda yanayokisiwa kuwa na uzito wa gramu 25 kila mfuko moja.
Kamanda Aziz alisema kuwa mashirikiano makubwa baina ya vijana wa ulinzi shirikishi wa shehia ya Maungani kwa kushirikiana na jeshi lake wameweza kufanikisha kukamatwa kwa mifuko hiyo inayosadikiwa kuwa ni madawa ya kulevya.
Alisema jeshi la polisi mkoa huo linamtafuta kijana Himirian ili aweze kuwajibika kisheria kutokana na kukutwa na vitu hivyo ambavyo ni dawa za kulevya aina ya bangi kinyume na saheria.
Kamanda Aziz alisema mara baada ya kumkamata kijana huyo atafikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria na kuchukuliwa hatua ili iwe funzo kwa watu wengine.
Aidha kamanda Aziz aliwapongeza vijana hao wa ulinzi shirikishi wa Shehia ya Maungani na kusema kwamba jeshi la polisi ni vyema likawaunga mkono kutokana na juhudi zao kwani inaaminika kuwa suala la madawa ya kulevya aina ya bangi hupitishwa katika njia za panya kupitia bandari bubu za maeneo hayo.
Hivyo aliziomba kamati za ulinzi, usalama na ustawi wa jamii wa Shehia hiyo kushirikiana na vijana hao kutokomeza matumizi ya dawa za kulevya katika mji wa Zanzibar.
Nae Sheha wa Shehia ya Maungani, Ali Kibwana Juma alithibitisha kutokea kwa tukio hilo huko katika shehia yake majira ya saa 7 kwenye nyumba ya mmiliki Zarnazi ambayo ilikutwa mifuko hiyo.
Hivyo Sheha Kibwana ameliomba jeshi la polisi kumaliza kituo cha polisi cha maungani ili kudhibiti matukio mbali mbali yanayojitokeza katika maeneo hayo kutokana na wahalifu wengi kutumia bandari zisizokuwa za halali ambazo ni bandari ya Kisakasaka na Nyamazi.
No comments:
Post a Comment