Habari za Punde

Nassari kuwapa wananchi fedha za mfuko wa jimbo

Joseph Ngilisho, ARUSHA


MGOMBEA Ubunge,katika jimbo la Arumeru Mashariki kupitia CHADEMA, Joshua Nasari amesema usiri wa Wabunge wa kushindwa kufichua na kuweka wazi matumizi ya fedha zinazotolewa kwa ajili ya maendeleo ya mfuko wa jimbo, unachangia umasikini kwenye majimbo.


Alisema Wabunge wengi wamekuwa hawatimizi wajibu wao kwa kushindwa kuwaeleza wananchi usahihi wa matumizi ya fedha hizo na badala yake zimekuwa zikitumika kinyume na makusudio, hali inayowafanya wananchi waendelee kuteseka.
Nassari alibainisha hayo katika kijiji cha Ngurdoto, akiwa kwenye mkutano wa kampeni wa kuomba kura kwenye uchaguzi mdogo wa jimbo la Arumeru Mshariki.


Mgombea huyo alisema mara nyingi wananchi hushindwa  kutambua fedha za mfuko wa jimbo na kujiuliza zinatolewa kwa ajili gani, hali ambayo kwa sasa imefanya hata baadhi yao kushindwa kujua maana halisi ya mfuko huo, kutokana na kugubikwa na usiri unaosababisha mianya wizi.


Alisema endapo atachaguliwa atahakikisha fedha hizo zinatumika kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya wananchi na kwamba hatakuwa Mbunge mbumbumbu na wala hatokuwa Mbunge anayelala na kusinzia akiwa Bungeni.


“Siombi kura kwa ajili ya kwenda kusinzia Bungeni, sitakuwa mbumbumbu nitajitahidi kuhakikisha natetea maslahi ya wananchi kwa wakati wote”,alisema Nasari.


Alisema kwa siku za nyuma katika jimbo hilo viongozi waliopita wakiwemo wabunge wameshindwa kutumia matumizi bora na yaliyokusudiwa katika mfuko huo hali ambayo mpaka sasa inasababisha jimbo hilo kuwa miongoni mwa majimbo ambayo hayana maendeleo huku rasilimali zikiwepo za kutosha.


“Kila mwaka zinatolewa milioni 47  kwa ajili ya mfuko wa maendeleo  jimbo lakini wananchi hawazioni matumizi yake na kuendelea kubeba changamoto za kijamii,  mimi napenda kuwaambia kuwa ni haki yenu ya msingi kuhakikisha kuwa mnajua maana halisi ya mfuko huu wa jimbo”, alisema Nassari.


Alisema kwa sasa jamii zinalia na watoto wa kike kupata ujauzito wakiwa katika masomo na wakiwa katika umri mdogo bila kujua sababu halisi kuwa ni hali ya maisha ambayo wanaishi watoto hao.


“Leo watoto wa kike wakipata mimba watu wanalalamika lakini wanashindwa kujua kuwa endapo kama Mbunge angetumia vema hata uongozi wake kwa kuboresha hata huduma ya elimu mimba zingekuwa si nyingi na mtoto wa jimbo hili anatembea umbali mrefu kuifuata skuli njiani anakumbana na vishwawishi hapa alaumiwe Mbunge na wala si mtu mwingine”, alifafanua Nassari.


Alifafanua endapo atashika nafasi hiyo ya uongozi katika jimbo hilo, fedha za mfuko wa maendeleo ya jimbo kwa kiwango kikubwa zitatumika kwa ajili ya maendeleo endelevu ya jamii.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.