Habari za Punde

Udhaifu wa Kutojua Haki za Wanawake Kisiwe Kigezo cha Kumdhalilisha

 Akielimishwa atajikomboa

Mwashamba Juma

LEO ni siku ya wanawake Duniani, wanawake wote ulimwenguni huisheherekea kwa kuikumbuka kwa furaha kwani iliweka bayana utu na hadhi kwa mwanamke.

Ni katika siku hii wanawake hujitathmini kwa mafanikio waliyofikia katika nyanja zote za kisiasa, uchumi, utamaduni na jamii kwa ujumla.

katika utekelezaji wa siku hii mataifa mengi ulimwenguni huitumia kama siku ya mapumziko kwao kwa kuzipongeza juhudi za wanawake katika maendeleo yao.


Maadhimisho ya siku hii yanakwenda sambamba na upingaji vikali wa udhalilishaji na ukatili dhidi ya jinsia ya kike, mateso na manyanyaso aliyobebeshwa mtoto wa kike katika kupambana na maisha ya kila siku.

Kwa upande wetu Tanzania siku hii tunaiadhimisha kwa kutoa jumbe mahususi ambao hushajihisha jamii na kuipokea siku hii na kujipongeza wanawake sote na hatua za maendeleo tulizopiga. ujumbe wa mwaka huu ni “ondoa ukatili dhidi ya wanawake Tanzania.”

Katika kuitekeleza kwa vitendo siku hii serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia wizara ya Ustawi wa Jamii Maendeleo ya Wanawake na Watoto imeunda sera ya “hifadhi maendelao ya wanawake.”
Katika utekelezaji wa sera hii Wizara ya Sheria, katiba na Utawala Bora inajukumu kubwa la kufahamisha jamii utekelezaji wa sera hii kisheria.

Kunachangamoto nyingi zinazowakabili wanawake ulimwenguni kote licha ya kuwa na makongamano, maadhimio, matamko pamoja na mikataba ya kimataifa lakini bado asilimia kubwa ya wanawake wanaendelea kunyanyaswa duniani kote, kulingana na tamaduni za mataifa husika.

Kwa upande wa mataifa yanayoendelea bado yanakabiliwana na changamoto nyingi katika nyanja zote za siasa, uchumi na utamaduni na jamii.

Katika nyanja za siasa na uchumi, kutokuwa na utulivu wa kisiasa kwa mataifa hayo kumeaathiri zaidi wanawake na watoto kwa kufanyiwa vitendo vya kinyama na kikatili.

Kesi za ubakaji mathalani hasa kwa wanawake na watoto bado ni changamoto kubwa katika mataifa hayo. Athari za ubakaji kama mimba pamoja na maambukizi ya maradhi kwa mfano maradhari ya kujamiiana, kisonono, kaswende na Ukimwi bado zinaendelea kuwa ni changamoto kwa wanawake walio wengi katika mataifa yanayoendelea.

Mataifa kama Misry, Sirya, Jamuhuri ya Demakrasia ya Kongo, Somalia, Palestina, Pakistan na kwengineko, vitendo hivyo vipo vingi kwa kuwadhalilisha wanawake kijinsia na kisaikolojia pamoja na kuwaharibia msimamo mzima wa maisha kwa kuwaekea historia mbaya za maisha pamoja na kuwabebesha mzigo mzito wa ugumu wa maisha kufuatia mizozo ya kisiasa isiyokwisha.

Udhalilishaji huo si tuu kwa nchi zenye vita, lakini pia nchi zenye sifa ya amani na utulivu wa siasa kama Tanzania, suala la ubakaji bado ni changamoto isiyokuwa na kikomo licha ya kuwa na makongamano, maadhimio, matamko pamoja na mikataba ya kimataifa lakina bado asilimia kubwa ya wanawake wanaendelea kunyanyasika hasa katika maeneo ya vijijini.

Kesi za ubakaji kwa wanawake na watoto wa jinsia zote zimekuwa kama ni shughuli kuu za kijamii badala ya kuunda mbinu ya kujiletea maendelea katika mataifa yetu.

Mwamko mdogo kwa wakaazi wa vijijini na uelewa hafifu wa umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike unaendelea kukwamisha maendeleo ya wanawake na kuupa kipaumbele mfumo dume ambao kwa miaka mingi unapigwa vita na mataifa yote ulimwenguni.

Fursa na haki ya kupata elimu kwa mtoto wa kike bado ni chamgamoto licha ya umasikini ulioukumba mataifa mengi yanayoendelea ambapo kwa kiasi kikubwa unaiathiri sekta ya elimu katika mataifa hayo na kupelekea kuzorotakwa sekta hiyo.

Hivyo hupelekea utegemezi kwa mwanamke na kumtengenezea mazingira ya nyanyasaji mtoto wa kike kwa kile kinachoaminika na kujuulikana kama ni tegemezi kwa mwanamme.

Aidha mbimba za utotoni ambazo zinakwamisha maendeleo na kudumaza utu wa mwanamke pamoja na kumdidimiza mwanamke katika shimo la umasikini asio utarajia, kwa kumbebesha mzigo mzito wa ulezi akiwa katika umri mdogo napengine kutelekezwa na familia ya watoto bila msaada wowote kutoka kwa baba wa watoto hao, huu ndio udhalilishaji wenyewe ambao daima wanawake tunaupiga vita.

Biashara ya uuzaji watu (Human traffics) bado ni changamoto kwa wanawake kwani wao ni waathirika wakubwa katika biashara hizo ambapo husafirishwa mbali ya mataifa yao kwa kuahidiwa kazi nzuri, kupatiwa elimu na maisha ya kifahari na badala yake kuambulia kazi nzito za majumbani, vibarua kwenye mashamba, pamoja na kushirikishwa kwenye biashara za ukahaba na ngono.

Wahusika wakuu kwenye biashara hizi aidha wanawake wenyewe, rafiki ama ndugu wa karibu wa familia za waathirika wa biashara hiyo.

Mataifa kama nchi za Mashariki ya kati, bara la Afrika, bara la Ulaya na Marekani ya Kaskazini biashara za kuuza watu zimeshamiri.

Machi 8 ya kila mwaka inapinga vikali dhidi ya udhalilishaji wa kimaumbile na kisaikolojia kwa wanawake wote ambao ni waathirika wakuu wa vitendo vya aina hiyo.

Zaidi ya miaka 100 imepita tokea kuwepo kwa dhana ya siku ya mwanamke duniani, lakini pia ni miaka 57 imepita tokea Umoja wa Mataifa kusaini mkataba wa kimataifa wa haki za wanawake huko San Franciscisco Marekani ili kuwapa fursa wanawake wote kusimama kidete na kutetea haki zao kisheria.

Mkataba wa mwaka 1945 ulikuwa ni mkataba wa mwanzo uliokemea udhalilishaji na ukandamizaji wa utu na hadhi ya mwanamke pamoja na kutetea haki zao dunia kote.

Lakini pia jumuiya hiyo ilianzisha sera na sheria za kimataifa kwa kuzifanya nchi wanachama kuunda sheria kwa mujibu wa sheria za nchi zao kwa lengo la kulinda hadhi ya mwanamke duniani, kuandaa progamu pamoja na kupitisha matamko mbalimbali juu ya haki za binaadamu katika kuutetea usawa wa mwanamke katika jamii.

Maadhimisho ya siku hii ni jukumu la Umoja wa Mataifa (UN) katika kukuza na kulinda pamoja na kutekeleza kwa vitendo haki sawa kwa wanawake duniani kote.

Licha yakuwa mataifa yametofautiana katika nyanja nyingi za kiutamaduni, rangi, dini, lugha, makabila, siasa na uchumi pamoja na kutenganishwa kwa mipaka ya mataifa yao lakini bado wanawake hao husimama kidete na kuwa kitu kimoja katika kuiadhimisha siku hii adhimu kwao kwa kupigania haki, amani na maendeleo katika jamii zao.

Siku hii pia huonesha msimamo imara kwa dada zetu wa nchi zinazopiganwa vita kama Afughanstan, na kwengineko duniani ambayo huisheherekea kwa vitendo.

Nchi kama Bosnia, Serbia, Romania, Russia, Macedonia, Slovnia, Latvia, Lithuania, Slovakia, Slovenia, Croatia, Estonia, Hungary, Montenegro, Herzegovina, Brazil, Croatia, na Poland, huitumia siku hii kwa kupeana zawadi za mauwa ya aina mbalimbali pamoja na kupongeza kwa hatua za maendeleo waliyofikia katika kila mwaka.

Katika kuadhimisha siku hii wanawake nchini Ugiriki kufanya mgomo wa kijinsia kwa waume zao ili kupinga manyanyaso dhidi yao.

Nchini ya Ureno nako usiku wa siku hii husheherekea kwa kula chakula cha usiku na kusheherekea kwa sherehe nzito za pati usiku kucha.

Baada ya kuvunjika kwa umoja wa nchi zikizokuwa zikiongoza siasa za kijamaa, nchini Armenia, siku ya wanawake kwa upande wao waliisheherekea tarehe 7 April, ambapo wengi wa wanawake waliona umuhimu wa Machi 8 na kuendelea kuisheherekea.

Wafanyakazi wanawake nchini Pakistani wa sekta rasmi na zisizo rasmi huisheherekea na kuiadhimisha siku hii kwa kupigania kudai haki ha fursa zao licha ya ugumu wa tamaduni na mila zinazombana mtoto wa kike dhidi ya ukandwamizwaji wa mtoto wa kike katika taifa hilo.

Katika kupunguza wimbi la uzalilishaji na kushusha hadhi ya mwanamke mataifa yote ulimwenguni, serikali yetu ya Tanzania pamoja na aasisi nyengine za kiraia zitumie nyazifa zao kwa kuondosha kabisa uzalilishaji wa wanawake kwa kuwachukulia hatua za kisheria na kinidhamu wale wote watakao patikana ama kushutumiwa kufanya au kushiriki kwa njia yoyote katika kuwakandamiza wanawake ki mwili ama kisaikolojia.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.