Habari za Punde

Wasira Awacharukia Wanaojiita Watoto wa Nyerere.

Na Mustafa Leu, ARUMERU

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya CCM, Stephen Wasira, amewashangaa viongozi wa CHADEMA wanaojiita kuwa wao ni watoto wa muasisi wa taifa la Tanzania, Julius Nyerere.

Wasira alisema hao wanaojipachuka vyeo kuwa waototo wa Nyerere hawafanani na vitendo vya kiongozi huyo na kwamba wanatumia jina hilo ili kutaka kuwarubuni wapewe kura jambo ambalo wananchi wa 
Arumeru Mashariki kamwe hawawezi kudanganyika na hila hizo.

Mjumbe huyo alieleza hayo katika vijiji vya Shishiton na Leguluki, kwenye mbio za kumnadi mgombea wa CCM Sioi Sumari katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Arumeru Mashariki.
Wasira aliwaeleza wananchi wa vijiji hivyo kuwa, CHADEMA ni waongo na hawamuelewi Mwalimu Nyerere, hivyo yeye na wengine waliofanya kazi na Nyerere watasimamia kueleza ukweli kuhusu Mwalimu na sio CHADEMA ambacho ni chama cha watalii.

Alifahamisha kuwa hata Mwalimu Nyerere angekuwa hai, hakuna kiongozi wa CHADEMA akiwemo Vicent Nyerere angeliweza kuzungumza naye kwani bado ni watoto wadogo ikilinganishwa na hadhi ya kiongozi huyo.

“Hakuna mtu kutoka CHADEMA anayeweza kuja kueleza habari za Nyerere kwa usahihi, huo ni uongo, wanatumia jina la Mwalimu Nyerere kujitafutia umaarufu kama leo angelikuwepo asingelikubali jina lake litumiwe ovyo ovyo na watu wasiokuwa na staha kama anavyofanya Vicent”, alisema Wasira.

Wasira alisema wanafahamu matatizo yanayowakabili wananchi wa Arumeru Mashariki na hayawezi kutatuliwa kwa siku moja lakini yale masuali mtambuka serikali ya CCM itahakikisha inayatekeleza kwa maslahi ya wananchi wa jimbo hilo.

Aliwataka wananchi wawapuuze wale wanaoeleza kuwa kwa miaka 50 CCM haijafanya lolote huku twakimu zikionesha kuwa skuli, zahanati, na ujenzi wa miundombinu umeongezeka katika kipindi hicho ikilinganishwa na nchi ilikotoka.

Kuhusu madai ya ardhi ya Wameru, Wasira, alisema kuwa Wameru walimteua marehemu Japheti Kiriro, alitumwa kwenda UNO, ambae alikwenda kuzungumzia matatizo ya ardhi, leo inakuwaje aibuke mtu na adai anayafahamu matatizo ya Wameru.

Aliwaomba wananchi wa vijiji hivyo kumchagua kijana Sioi Sumari ambaye ndiye shupavu watakaeshirikiana na wananchi hao katika kuwaletea maendeleo yao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.