Habari za Punde

India Yasifu Mafanikio ya Kisiasa na Kiuchumi Zanzibar

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na balozi mdogo wa India aliyepo Zanzibar Bw. Dalip Singal aliyefika ofisini kwake Migombani kwa ajili ya kumuaga, baada ya kumaliza muda wake wa utumishi nchini.(Picha, Salmin Said, OMKR).

Na Hassan Hamad (OMKR).

India imesifu mafanikio ya kisiasa na kiuchumi yaliyopatikana Zanzibar tangu kuanzishwa kwa mfumo wa serikali ya umoja wa kitaifa.

Akizungumza na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad huko ofisini kwake Migombani, balozi mdogo wa India aliyepo Zanzibar Bw. Dalip Singal amesema Zanzibar imefanya mabadiliko makubwa ya kisiasa na kiuchumi ambayo yanapaswa kuendelezwa kwa maslahi ya nchi.


Balozi Singal ambaye alionana na Makamu wa Kwanza wa Rais kwa ajili ya kumuaga rasmi kufuatia kumaliza muda wake wa utumishi hapa nchini amesema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita ameshuhudia mabadiliko makubwa yakiwemo kuimarika kwa umoja wa wazanzibari.

Sambamba na hilo balozi Singal amesema Zanzibar imeweka mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji, na kuomba kuimarishwa kwa mazingira hayo, ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi kutoka nchini tofauti duniani.

Akizungumzia kuhusu uhusiano kati ya Zanzibar na India, balozi huyo amesema uhusiano wa kindugu na kihistoria uliopo unaendelea vizuri na unapaswa kuendelezwa kwa maslahi ya pande hizo mbili.

Amefahamisha kuwa katika kipindi chake cha uongozi pia ameshuhudia mambo kadhaa ya maendeleo yakiwemo kutiliana saini mikataba mbali mbali hasa katika sekta za elimu na afya, mambo ambayo yanakuza mahusiano na kuboresha huduma za kijamii.

Amesema licha ya uchumi wa Zanzibar kuonekana kuwa chini, lakini serikali inajitahidi kuweka miundombinu ya kukuza uchumi, hatua ambayo inaweza kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi katika siku zijazo.

Katika mazungumzo hayo balozi Singal amempongeza Makamu wa Kwanza wa Rais kwa kutembelea India na kubahatika kuonana na viongozi muhimu wa nchi hiyo, sambamba na kusifu mashirikiano aliyoyapata Zanzibar, na kwamba mambo hayo ni muhimu katika kuendeleza mahusiano na kukuza uchumi wa nchi husika.

Kwa upande wake Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema Zanzibar imenufaika sana kutokana na uhusiano wa kweli na India, na kuahidi kuendelezwa kwa uhusiano huo.

Amesema Zanzibar imekuwa ikinufaika kikamilifu kutokana na uhusiano wake na India kwa kupata nafasi nyingi za masomo, sambamba na ushirikiano wake katika sekta ya afya na sekta nyengine za maendeleo.

Kuhusu ziara yake ya India aliyoifanya mwezi Septemba mwaka jana, Maalim Seif amesema imeleta mafanikio kwa Zanzibar ikizingatiwa kuwa pamoja na mambo mengine walijifunza mbinu mbali mbali za kuendeleza shughuli za kiuchumi, sambamba na kutiliana saini makubalialo ya mashirikiano katika nyanja tofauti za kiuchumi.

Amesema serikali imewaka utaratibu maalum wa kufuatilia utekelezaji wa makubaliano yaliyofiwa baina ya India na Zanzibar na kumtaka balozi huyo kukumbushia makubaliano hayo wakati atakaporejea, ili kusaidia kutoa msukumo wa utekelezaji wake.

Amesema kwa sasa Serikali inaendelea kujipanga kuialika timu ya wataalamu wa afya kutoka hospitali ya Apollo nchini India kuja kutoa huduma zao hapa Zanzibar, ili kurahisisha upatikana wa huduma za dharura za afya kwa wananchi, badala ya wananchi kuzifuata huduma hizo nchini india, jambo ambalo linaleta usumbufu.

Balozi Singal anastaafu kazi baada ya kulitumikia taifa lake kwa kipindi cha miaka 40.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.